BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Mwandishi Wetu, Mbeya
MBEYA City leo imefanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mwadui katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom uliochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Mwadui licha ya kuwa ugenini walitawala mchezo huo katika kipindi cha kwanza huku wakifanya mashambulizi kadhaa ambayo hayakuzaa matunda.


City walipata bao lao dakika ya 49 mfungaji akiwa Ditram Nchimbi aliyekokota mpira na kuubetua kiufundi mpira huo uliompita juu kipa wa Mwadui, Shaban Kado.

Katika mchezo huo kiungo Haruna Moshi 'Boban' alitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kujidondosha kwenye eneo la hatari la Mwadui hiyo ikiwa ni kadi ya pili ya njano baada ya kuonywa hapo awali.

Boban (aliyekaa) akilalamika baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu

Michezo mingine iliyochezwa leo, Mgambo JKT imeifunga JKT Ruvu bao 5-1, Majimaji nayo ikiwa ugenini imepata sare ya bao 1-1 dhidi ya Coastal Union mechi iliyochezwa uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Prisons ya Mbeya ilisafiri mpaka jijini Mwanza kuifuata Toto African na kupata ushindi wa bao 1-0 huku Stand United ya Shinyanga nayo imeifunga Kagera Sugar bao 1-0, mechi iliyochezwa uwanja wa Kambarage mkoani humo.

Usiku wa leo katika Uwanja wa Chamazi, Azam Fc wao wataikaribisha African Sports ya jijini Tanga.

Post a Comment

 
Top