BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
MICHUANO ya kombe la Mapinduzi imeendelea usiku huu kwa mchezo mmoja uliozikutanisha Mtibwa Sugar na Azam FC. Mechi hiyo iliyochezwa katika uwanja wa Amaan ilimalizika kwa sare ya bao 1-1.

Mtibwa iliyokuwa na nyota wake wote ilitawala mchezo huo kwa asilimia kubwa huku wakitengeneza nafasi kadhaa ambazo washambuliaji wake walikosa umakini hivyo kupelekea dakika 45 za kwanza za mchezo huo zikimalizika huku timu hizo zikiwa hazijafungana.Kipindi cha pili Mtibwa waliendelea kuliandama lango la Azam ambayo ilionyesha wazi kuzidiwa kila kitu katika mchezo huo. Mashambulizi hayo yalizaa matunda katika dakika ya 60 baada ya Hussein Javu kuipatia Mtibwa bao la kuongoza.

Kuingia kwa John Bocco na Kipre Tchetche kuliipa uhai Azam ambapo katika dakika ya 73, Bocco aliupenya ukuta wa Mtibwa na kuingia katika eneo la penati ambapo walinzi wawili wa Mtibwa walimfanyia madhambi na mwamuzi kuamuru ipigwe penati iliyokwamishwa nyavuni na Bocco mwenyewe katika dakika ya 74.

Mechi hiyo iliingia dosari katika dakika za majeruhi pale Issa Rashid 'Baba Ubaya' alipowapita walinzi wa Azam na kupiga krosi iliyomaliziwa nyavuni na Ramadhan Kichuya lakini mwamuzi wa pembeni akakataa bao hilo kwa madai kuwa mfungaji alikuwa ameotea. Hata hivyo, marudio ya picha za video yalionyesha wazi hakukuwa na mtu aliyeotea.

Michuano hiyo itaendelea kesho ambapo URA itapepetana na JKU katika mechi ya jioni itakayofuatiwa na Jamhuri dhidi ya Simba usiku.

Post a Comment

 
Top