BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
BAADA ya jana usiku kutangazwa kuwa straika wa TP Mazembe na Taifa Stars, Mbwana Samatta ndiye Mchezaji Bora Afrika kwa wachezaji wa ndani baba mzazi wa mchezaji huyo, Ally Mohamed Samatta alijikuta akiangua kilio kilichopelekea kuwaamsha majirani na watoto wake wakidhani kwamba kuna tatizo limempata.Akizungumza na BOIPLUS, Mzee Samatta alisema alijikuta akiangua kilio cha furaha huku mke wake Khadija Abdallah akipandwa na presha kwa kutoamini kilichotokea usiku wa jana.

''Nimefurahi sana mpaka muda huu mwanangu kupiga hatua kubwa katika soka, Samatta ameiwakilisha vyema nchi yake na watanzania kwa ujumla. Nimelia sana jana usiku kwani sikuamini kilichotokea, nimelala alfajiri ya saa 11 na nimeamka saa moja asubuhi jambo ambalo si la kawaida kwangu, tuliyoomba kabla ya kwenda huko yametimia ni jambo la kumshukuru Mungu.

''Kabla ya kuondoka nilimuahidi kumuandalia sherehe endapo atashinda sasa imekuwa hivyo tutafanya sherehe ya kumpongeza kama wana familia. Yeye alitaka tufanyie hapa hapa nyumbani lakini haitawezekana kwasababu eneo ni dogo lazima twende sehemu ya kujitanua,'' alisema Mzee Samatta.

Baba huyo aliendelea kuweka wazi kuwa Samatta anabarikiwa na kufunuliwa neema kwenye mambo yake kwa sababu ana nidhamu na anamshirikisha Mungu kwa kila jambo lake na ndiyo maana ameamua kubomoa nyumba yake nyingine iliyopo Saku, Maji Matitu na anataka kujenga msikiti.

''Achana na nyumba anayobomoa kule Kibada kuna nyumba nyingine aliinunua huko Maji Matitu ameishaibomoa bado tu hajaanza ujenzi kwani hapo amepanga kujenga Msikiti jambo ambalo ni la kheri na baraka kwake katika kuongeza mafanikio,'' alisema

Samatta ni miongoni mwa wachezaji wenye mafanikio makubwa Tanzania ukiachana na Afrika Mashariki na Kati ambapo amefanikiwa kuwekeza kwa asilimia kubwa kwenye ardhi na nyumba.

Samatta alikuwa na nyumba saba ambapo moja aliuyojenga Mbande aliamua kuuza baada ya kujengwa chini ya kiwango, nyingine ni hiyo aliyobomoa kwa ajili ya ujenzi wa Msikiti na hivyo amebaki na nyumba tano ikiwemo ya Kibada anayoibomoa kwa ajili ya kujenga ghorofa la kisasa.

Kwa mujibu wa Mzee Samatta, amesema mwanaye amewekeza pia kwenye viwanja ambapo ana viwanja zaidi ya 10 pamoja na mashamba zaidi ya matatu huku pia akimiliki  magari ya kifahari.

Post a Comment

 
Top