BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
KLABU ya Simba leo mchana imevunja rasmi mikataba ya makocha wao Dylan Kerr na kocha wa makipa Idd Salim katika kikao cha Kamati ya Utendaji na sasa timu hiyo itakuwa chini ya kocha msaidizi, Jackson Mayanja raia wa Uganda.


Kikao hicho kinachoelezwa kuongozwa na Rais wa Simba, Evans Aveva kiliwaita makocha hao waliokuwa Zanzibar ambapo wameingia leo asubuhi na kwenda moja kwa moja kikaoni ambako walitakiwa kujieleza pia.

Baada ya majadiliano hayo kwa pamoja wameamua kuvunja mikataba hiyo kwa faida ya pande zote mbili huku habari kutoka ndani ya kikao hicho zikieleza kuwa tayari kuna majina matatu ya makocha waliopendekezwa kumrithi Kerr yanajadiliwa.

Msemaji wa Simba, Haji Manara amethibitisha kuvunjwa kwa mikataba ya makocha hao na kwamba mchakato wa kumpata kocha mwingine unaendelea.

Baada ya mechi ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi ambapo Simba ilitolewa na Mtibwa Sugar kwa bao 1-0, kocha wa makipa alijikuta akitiwa kwenye vyombo vya dola baada ya kumpiga shabiki huku Kerr akidaiwa kumrushia maneno makali kocha wa Taifa Stars, Boniface Mkwassa.

Kitendo hicho kimechangia viongozi wa Simba kuchukia mbali na kutoridhishwa na mwenendo wa kikosi chao.

Post a Comment

 
Top