BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Mwandishi Wetu
KIUNGO Haruna Niyonzima ameomba radhi uongozi na wanachama wa Yanga huku akisema amewasamehe wale waliomkosea ili maisha yaendelee.


Mwezi uliopita, Yanga ilitangaza kuvunja Mkataba na Nahodha huyo wa Rwanda kwa tuhuma za kukiuka vipengele vya Mkataba wake.
Lakini leo katika Mkutano na waandishi wa habari makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam, Niyonzima ametangaza kukiri kosa la kushindwa kutoa taarifa ya matatizo yake kwa wakati na kuomba radhi .

“Ninapenda kuchukua fursa hii kuomba msamaha kwa uongozi na wanachama wa Yanga, ni kweli nilishindwa kutoa taarifa mapema juu ya matatizo yangu, naomba wanisamehe,”

"Nami kwa upande wangu nimewasamehe wote walionikwaza katika hili lililoniletea matatizo na klabu yangu." alisema Niyonzima

Aidha, Niyonzima amesema kwamba kulitokea kutoelewana kimawasiliano na ofisi ya Katibu Mkuu, Dk Jonas Tiboroha kiasi cha kulifikisha suala hilo kwenye hatua hiyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, Jerry Muro amesema kwamba suala la Niyonzima limefika katika uongozi mkuu wa klabu na lipo katika hatua nzuri ya kufikia muafaka huku akisisitiza klabu itatoa taarifa ya maandishi.

Ingawa Muro hakuweka wazi, lakini inavyoonekana Yanga imeshamalizana na mchezaji huyo na kwamba muda si mrefu itatangaza rasmi kumrejesha kundini kipenzi hicho cha wanayanga.  


Yanga ilitangaza kuvunja Mkataba na Niyonzima baada ya kuchelewa kurejea klabuni kufuatia kuruhusiwa kwenda kuichezea Rwanda katika Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki, 'CECAFA Challenge' nchini Ethiopia Novemba.

Awali, Yanga SC ilimsimamisha kwa muda usiojulikana Niyonzima kabla ya suala lake kupelekwa Kamati ya Nidhamu, ambayo hatimaye ilichukua maamuzi hayo yaliyowashtua wanayanga.

Post a Comment

 
Top