BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
STRAIKA wa TP Mazembe na timu ya taifa ya Tanzania, Mbwana Samatta ameamua kubomoa nyumba yake mpya aliyoijenga huko Kisarawe mkoani Pwani kwa madai kwamba haikuwa na nafasi aliyotaka na amepanga kujenga nyumba ya kisasa zaidi.

Samatta amefanya jambo ambalo limewashangaza wengi ila yeye mwenyewe amesema amefanya ili kuuridhisha moyo wake kwa maana ya kuupa kile unachotaka.


Samatta alikuwa ameshakamilisha ujenzi wa nyumba hiyo lakini ghafla akawaagiza mafundi waibomoe mara moja ili aanze ujenzi wa nyumba nyingine itakayokuwa katika mtindo autakao.


BOIPLUS iliamua kumsaka mfungaji bora huyo wa ligi ya Mabingwa Afrika ili athibitishe taarifa hizo ambazo walioshuhudia tukio wanasema hawakuamini macho yao, Samatta alikiri kubomoa nyumba hiyo ingawa alistaajabu kusikia mwandishi wa habari hizi amejua jambo ambalo yeye amelifanya kwa siri kubwa.

"We umepata wapi taarifa hizo? (Huku akicheka).
Ni kweli nimeibomoa kaka, ilikuwa nyumba nzuri sana ila ndani haikuwa na nafasi kama vile nilivyotaka, kwahiyo nitaanza ujenzi wa nyumba ya kisasa zaidi". Alisema SamattaNyumba hiyo iliyobomolewa ambayo Samatta anadai ingemnyima 'kujinafasi' kama anavyotaka ilikuwa na vyumba vinne vya kulala na sasa kuna taarifa kuwa amepanga kujenga ghorofa.

Samatta anakaribia kujiunga na KRC Genk inayoshiriki ligi kuu nchini Ubelgiji akitokea Mazembe katika uhamisho ambao utawagharimu Genk kiasi cha Euro 2.5 milioni (Zaidi ya Sh 6 bilioni).

Post a Comment

 
Top