BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
MAMBO yameshanoga kwa mtanzania Mbwana Samatta aliye kwenye hatua za mwisho kujiunga na KRC Genk ya nchini Ubelgiji akitokea TP Mazembe ya DR Congo.


Baada ya kutua salama Genk jana, straika huyo atafanyiwa vipimo vya afya leo ijumaa wakati mmiliki wa Mazembe, tajiri Moise Katumbi akipasua anga kwenda kukamilisha uhamisho huo.

"Nimefika salama bro, kesho (leo) nitafanyiwa vipimo vya afya huku tukimsubiri Katumbi aingie kutoka Lubumbashi kwa ajili ya kumalizia taratibu za mwisho kabla sijatambulishwa rasmi." alisema Samatta

Samatta akifuzu vipimo vya afya atabaki akimsubiri Bosi wake huyo atue Ubelgiji na kumalizia mazungumzo na mabosi wa Genk kabla hajasaini mkataba ambao utakuwa na kipengele cha Mazembe kulipwa asilimia 20 ya ada ya uhamisho kama Genk itamuuza Samatta kwenda timu nyingine.

Simba ya jijini Dar es Salaam nayo iliweka kipengele kama hicho wakati walipomuuza kwenda Mazembe na sasa wanamsubiri Katumbi atoke Ubelgiji awape chao.

Wakati huo huo, watanzania waishio nchini humo wameonyesha kufurahishwa sana na usajili wa nahodha huyo wa Taifa Stars huku wakiahidi kuanza kuhudhuria mechi za Genk ili kutoa 'support' kwa nyota huyo.

Wakizungumza na BOIPLUS kwa nyakati tofauti, watanzania Kahema Kivaria na Nyambi Kop Lunyasi walisema kwa wanavyoijua Genk, Samatta atafanya vizuri na hiyo itakuwa ni kama njia yake ya kuyafikia mafanikio. Pia walielezea hisia zao kuwa wanatamani wawepo wakati wa utambulisho wa mchezaji huyo.

Post a Comment

 
Top