BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
MCHEZAJI Bora wa Afrika kwa ligi ya ndani na mfungaji bora wa ligi ya Mabingwa Afrika, Mbwana Samatta, kesho atakwea pipa kwenda nchini Ubelgiji katika klabu ya KRC Genk kwa ajili ya kuanza kuitumikia kama mchezaji wa kulipwa.Hatua hiyo imefikia baada ya msuguano wa muda mrefu kati ya Samatta na Moise Katumbi ambaye ni mmiliki wa TP Mazembe klabu aliyokuwa akiichezea, juu ya timu gani aende. Katumbi alikuwa akisisitiza mtoto huyo wa Afisa mstaafu wa jeshi la Polisi aende Nantes ya Ufaransa wakati Samatta akiwa ameshamalizana na Genk.


Akizungumza na BOIPLUS jioni ya leo, Samatta alikiri kumalizana na Katumbi na kwamba sasa anaondoka kwenda kuanza maisha mapya barani Ulaya na kwamba akifika kule kitakachosubiriwa ni ukamilishwaji wa uhamisho huo kwa njia ya mtandao 'Transfer Matching System (TMS)' 


"Nashukuru Mazembe nimemalizana nao vizuri, kesho nitaondoka kwenda Ubelgiji, kwa upande wangu mimi nilishamalizana na Genk, kinachobaki ni Mazembe kukamilisha uhamisho kwenye TMS." alisema Samatta


Katika hatua nyingine vigogo wa Ufaransa Olympic Marseille ambao mwishoni mwa wiki iliyopita walionyesha nia ya kumhitaji Samatta, wameendelea kushikilia msimamo wao licha ya kuelezwa kuwa straika huyo ameshamalizana na Genk.


"Marseille bado wanasema wananihitaji, nimewaambia wakazungumze na Genk kwanza kwavile nimeshasaini nao mkataba wa awali na sitaki kuwa kinyonga. Na hii ni kwavile mimi sitaki kujihusisha na hii vita, nimewaachia wenyewe huko, mimi naenda Ubelgiji." alifafanua Samatta

Post a Comment

 
Top