BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
IFIKAPO saa 4:30 usiku wa leo, kituo cha Televisheni cha Super Sport kupitia chaneli yake ya Super Sport 4 kitarusha moja kwa moja sherehe za utoaji wa tuzo za Afrika zinazofanyika Abuja, Nigeria.


Kwa mara ya kwanza, Tanzania imepata mwakilishi ambaye ni Straika wa TP Mazembe, Mbwana Samatta. 
Straika huyu ameingia kwenye tatu Bora akiwania tuzo ya mchezaji Bora wa Afrika anayecheza ligi za ndani baada ya kuisaidia Mazembe kutwaa ubingwa wa Afrika huku yeye akiibuka mfungaji Bora wa michuano hiyo.

Samatta ana nafasi kubwa ya kutwaa tuzo hiyo ila ni wajibu wetu watanzania kumuombea afanikiwe ili taifa letu lianze kuonekana kwenye ramani ya soka barani Afrika na duniani kwa ujumla.

Samatta ameiambia BOIPLUS kuwa anawashukuru sana watanzania kwa jinsi wanavyomuonyesha upendo hasa katika kipindi hiki kuelekea utoaji wa tuzo hizo.

"Waambie watanzania nawashukuru sana kwa upendo wao, napokea meseji nyingi za kunitakia heri, nafarijika sana na nafurahi kuwa mmojawao. Wasiache kuniombea ili nifanikiwe". Alisema Samatta akiwa katika Hoteli ya Hilton alipofikia.


Kama Samatta atatwaa tuzo hiyo basi atakuwa ameweka rekodi nyingine ya kuwa mtanzania wa kwanza kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika kwa wanaocheza ligi za ndani. Rekodi nyingine ambayo yeye na Thomas Ulimwengu waliiweka kwa pamoja ni ile ya kuwa Watanzania wa Kwanza kutwaa Kombe la Ubingwa wa Afrika baada ya timu yao, Mazembe, kubeba kombe hilo Novemba 8 mwaka jana.

Post a Comment

 
Top