BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
UCHU wa mabao ulioonyeshwa na wachezaji wa Simba leo umewafanya mashabiki wao waanze kupata matumaini ya kuiona tena ile timu yao iliyokuwa ikiitwa 'Simba Dozi'. Hiyo ni baada ya timu hiyo kuibamiza African Sports mabao 4-0 katika mchezo wa Ligi kuu ya Vodacom uliochezwa katika dimba la Taifa.


Hamis Kiiza alianzisha karamu hiyo ya mabao baada ya kuifungia Simba bao la kwanza katika dakika ya 14 kabla Hassan Kessy hajaupangua ukuta wa Sports na kuipatia Simba bao la pili katika dakika ya 31.

Kuonyesha walipania kushinda mabao mengi, Simba waliendelea kuliandama lango la Sports na katika dakika ya 43, Kiiza tena aliwafurahisha mashabiki wao kwa kufunga bao la tatu baada ya kuwatoka walinzi pamoja na golikipa Zakaria Mwaluko.

Kipindi cha pili kilianza kwa Sports kumiliki mpira huku wakijaribu kulifikia lango la Simba lakini uimara wa mabeki Juuko Murshid na Hassan Isihaka uliwanyima nafasi ya kumsabahi mlinda mlango Vicent Angban.


Kinda anayekuja kwa kasi katika safu ya ushambuliaji ya Simba, Hija Ugando alifungua akaunti yake ya mabao katika Ligi kuu baada ya kuipatia timu yake bao la nne katika dakika ya 75 akitumia uwezo binafsi wa kukokota mpira katikati ya mabeki kabla hajamchambua kipa wa Sports.

Kwa matokeo haya Simba imefikisha pointi 36 ikiwa ni pointi tatu nyuma ya Azam na Yanga iliyopoteza mchezo wake wa leo dhidi ya Coastal Union kwa kufungwa mabao 2-0. Mabao ya Coastal yamefungwa na Miraji Adam na Juma Mahadhi.

Katika michezo mingi ya ligi kuu iliyopigwa leo, Mwadui imeifunga Toto bao 1-0 huku mechi ya Mtibwa Sugar na Stand Utd imevunjika Mtibwa ikiongoza kwa bao 1-0 katika dakika ya 75 baada ya uwanja kujaa maji kutokana na mvua kubwa iliyonyeesha, hivyo watacheza kesho asubuhi kumalizia hizo dakika 15.

Post a Comment

 
Top