BOIPLUS SPORTS BLOG

IKIWA inacheza soka lisilo na mipango, kukiwa hakuna nia ya kutafuta goli wala hatari za maana katika lango la wapinzani, Simba imejikuta ikipokea kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar na kuaga mashindano ya kombe la Mapinduzi.Nyota wa Mtibwa iliyokuwa bora uwanjani alikuwa Ibrahim Jeba aliyefunga bao safi katika dakika ya 45 akitumia vizuri uzembe wa kipa wa Simba, Manyika Peter aliyeshindwa kuficha shuti la Shiza Kichuya na kupangua kizembe mbele ya Jeba.

Simba licha ya kucheza na viungo wanne Justice Majabvi, Awadhi Juma, Jonas Mkude na Mwinyi Kazimoto ilishindwa kucheza soka la kivutia katika dakika 80 za mchezo na kuonekana hatari katika dakika 10 za mwisho. Viungo wa Mtibwa wakiongozwa na mkongwe, Shaban Nditi walifanikiwa kulikamata dimba la kati kisawasawa mbele ya viungo hao ghali zaidi nchini.


Mshambuliaji wa Simba, Danny Lyanga alijikuta akimaliza mechi ya sita bila kufunga bao wakati Mkenya Raphael Kiongera aliyeingia kipindi cha pili akimaliza mechi saba bila kufunga bao hata la kuotea hivyo kukiweka shakani kibarua cha kocha wao Mwingereza, Dylan Kerr.

Mabeki wa Simba, Juuko Murshid, Hassan Isihaka na Mohamed Hussein walionekana kama hawako mchezoni na kufanya makosa ya mara kwa mara na kama wachezaji wa Mtibwa wangekuwa makini wangeweza kupata mabao mengi zaidi.

Mtibwa sasa inasubiri mshindi kati ya Yanga na URA katika mechi ya fainali itakayochezwa Jumatano ya wiki hii.

Post a Comment

 
Top