BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Akram Msangi 'Mido'
MCHEZAJI wa Simba, Joseph Kimwaga leo alikusudia kuvunja mkataba na klabu hiyo kwa kile alichodai kuwa hawezi kuvumilia tabia za ubaguzi zinazoendelea ndani ya timu hiyo lakini viongozi wake wamemtuliza na kumwambia lazima atacheza tu.


Kimwaga aliiambia BOIPLUS kuwa wakati kocha Dylan Kerr yupo ndani ya Simba alikuwa hapewi nafasi ya kucheza lakini ameondoka na kuja Jackson Mayanja hali hiyo imeendelea kwani ameondolewa kwenye kambi ya wachezaji 18 watakaoivaa Mtibwa Sugar kesho.

Kimwaga alisema kuwa hafurahishwi na tabia hizo na kwamba alikuwa akimchukia Kerr kumbe tatizo ni la viongozi ambao walifikia hatua ya kumpangia kikosi huku wakitaka yeye asipangwe.

"Nilikuwa na lengo hilo na nimemfuata Rais Evans Aveva kwa lengo la kuvunja mkataba wangu lakini ameniambia suala langu litatatuliwa na nitapata nafasi ya kucheza kwani huyu ni kocha mwingine.

"Hivyo nasubiri kuona mabadiliko hayo kama nicheza ama lah. Jambo ambalo silitaki ni hilo kwani kiwango changu kinashuka," alisema Kimwaga.

Simba ina mechi ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo watakutana na Mtibwa Sugar waliowafunga kwenye hatua ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi.

Post a Comment

 
Top