BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda


WEKUNDU wa Msimbazi Simba SC leo wameibuka na ushindi wa bao 1-0  pale ilipopepetana na watoza ushuru wa Uganda, URA, katika uwanja wa Amaan kwenye mechi ya kundi A ya kombe la Mapinduzi.

Ilionekana kama vile kipindi cha kwanza kingemalizika bila timu yoyote kupata bao kutokana na mchezo huo kuchezwa zaidi eneo la kati la uwanja huku mashambulizi mengi yakiwa ni yale yasio na tija, lakini Ibrahim Ajibu alibadili kila kitu kwa bao lake safi la dakika ya 37 baada ya kupiga shuti kali.

Kipindi cha pili Simba iliyofikisha pointi nne ilifanya mashambulizi kadhaa ya maana lakini 'uchoyo' wa Danny Lyanga uliwanyima mabao mawili ya wazi vijana hao wa mtaa wa Msimbazi.

Simba walioonyesha kiwango safi ukilinganisha na mchezo uliopita, waliliandama lango la URA katika dakika za mwisho za mchezo huo ingawa washambuliaji wake walikosa umakini hivyo kuinyima mabao zaidi timu yao.

Simba itamaliza mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi siku ya Ijumaa kwa kucheza na JKU huku Jamhuri wakiumana na  URA.

Post a Comment

 
Top