BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Swabri Kachwamba
KAGERA Sugar wameamua kuhama Uwanja wao wa nyumbani wa Ally Hassan Mwinyi uliopo Tabora na sasa mechi zao mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara zitachezwa Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga.

Uamuzi huo umetokana na kupata matokeo mabovu mfululizo kwenye Uwanja huo na hivyo wanaamini kwamba mabadiliko hayo yanaweza kubadili matokeo yao.


Kwa maana hiyo, mechi yao na Simba ambayo ilipangwa kuchezwa Tabora itachezwa Shinyanga ambapo Simba watalazimika kucheza mechi zao mbili mfululizo kwenye uwanja huo, wataanza na Kagera Sugar na kumalizia dhidi ya Stand United.

Nahodha wa timu hiyo, George Kavilla amethibitisha juu ya hilo, "Labda kule hatukuwa na bahati tumeona tuhamie hapa Shinyanga, matokeo yetu yanakatisha tamaa ila hatuwezi kushuka daraja. Tutapambana kuhakikisha tunabaki kwenye ligi.

"Tunacheza vizuri ila tunashindwa kufunga, nafikiri kuna mambo mengi tu yanaendelea ambayo tunatakiwa kuyafanyia kazi haraka ili mechi zijazo tufanye vizuri, huwa tunaumia sana kuona hali hii inatutokea,"  alisema Kavilla.


Kagera Sugar imekuwa ikihamahama Uwanja baada ya Uwanja wa Kaitaba ambao wanautumia kama uwanja wao wa nyumbani kuanza matengenezo na sasa upo katika hatua za mwisho ili ukabidhiwe kwa ajili ya matumizi.

Post a Comment

 
Top