BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
USHINDI wa bao 1-0 walioupata Simba leo dhidi ya JKU ni kama vile wamewakimbia watani zao wa jadi,Yanga ambao wamemaliza wakiwa vinara wa kundi B.
Mechi hiyo imechezwa katika dimba la Amaan.

Bao pekee la Simba liliwekwa nyavuni katika dakika ya 65 na Jonas Mkude kwa kichwa akimalizia krosi safi ya beki wa kulia Emery Nimubona ambaye ameonyesha kiwango cha juu katika michuano hii ya kombe la Mapinduzi.


Simba walitengeneza nafasi kadhaa katika kipindi cha kwanza lakini washambuliaji wake walishindwa kuzitumia nafasi hizo. Kipindi cha pili kocha Dylan Kerr aliamua kuwapumzisha Hamis Kiiza, Awadh Juma na Paul Kiongera huku nafasi zao zikichukuliwa na Mwinyi Kazimoto, Ibrahim Ajib na Danny Lyanga.

Mabadiliko haya yalibadili hali ya mchezo kiasi cha kuifanya Simba ihamishie kambi langoni mwa JKU lakini bado washambuliaji hawakuweza kuziona nyavu za JKU hadi kiungo Mkude alipofanya hivyo.

Kwa matokeo hayo Simba imeongoza kundi A hivyo itaumana na Mtibwa siku ya jumapili saa 10:15 alasiri huku Yanga wao wakipepetana na URA siku hiyo hiyo saa 2:15 usiku.
Fainali ya michuano hii itapigwa siku ya jumanne.

Post a Comment

 
Top