BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
SIMBA leo imelipa kisasi kwa kuifunga Mtibwa Sugar bao 1-0 ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Wiki iliyopita Mtibwa Sugar waliiondoa Simba kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi katika hatua ya nusu fainali kwa bao 1-0.Simba ilipata bao hilo pekee dakika ya tano lililofungwa na mshambuliaji wao Hamisi Kiiza akiitumia vizuri krosi safi ya Mohamed Hussein 'Tshabalala' akiwa amefikisha mabao tisa.

Dakika ya 18, Kiiza alikosa bao baada ya kupiga shuti kali lililotoka nje kidogo ya goli huku Mwamuzi wa mchezo huo Ahmada Simba akimpa kadi ya njano kiungo wa Mtibwa Sugar, Henry Joseph kwa kumchezea rafu Peter Mwalyanzi wa Simba ikiwa ni dakika ya 31.

Kipindi cha kwanza Simba ilicheza kwa kiwango cha juu ambapo ilikuwa ikishambulia lango la Mtibwa mara kwa mara ingawa walishindwa kutumia vyema nafasi walizozipa huku Kiiza akikosa tena bao dakika ya 33 baada ya kupiga shuti na kutoka nje.

Kocha wa Mtibwa Sugar, Mecky Mexime alifanya mabadiliko kwa kuwatoa Hussein Javu na Mohamed Ibrahim ambao nafasi zao zilichukuliwa na Jaffer Kibaya pamoja na Vincent Barnabas.

Kocha wa Simba, Jackson Mayanja naye akimtoa Ibrahim Ajibu na Kiiza  nafasi zao zilichukuliwa na Danny Lyanga pamoja na Awadhi Juma.Ajibu hakuweza kuendelea na mchezo baada ya kuumia na kulazimika kutolewa nje kabisa ya uwanja kwa machela kwa ajili ya kupata huduma ya kwanza.

Dakika ya 73, mwamuzi alilazimika kutoa kadi ya njano kwa Said Ndemla baada ya kumchezea rafu mchezaji wa Mtibwa Sugar, Barnabas.

Kwa matokeo hayo Simba imefikisha pointi 30 na imebaki nafasi ya tatu ikiwa nyumba ya Azam wenye pointi 35 na Yanga yenye pointi 33.

Post a Comment

 
Top