BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
TIMU ya Simba ya jijini Dar es Salaam leo imeshindwa kuitambia Jamhuri ya Wete, Pemba, baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 katika mchezo wa kuwania Kombe la Mapinduzi uliopigwa katika uwanja wa Amaan.


Simba ndio walianza kulifikia lango la Jamhuri ambapo washambuliaji wake Hija Ugando, Paul Kiongera na Joseph Kimwaga walipoteza nafasi kadhaa za kuipatia timu hiyo mabao ya mapema.

Dakika ya 12 Awadh Juma aliipatia Simba bao la kuongoza kwa shuti kali la nje ya 18 ambalo licha ya mlinda mlango wa Jamhuri, Omari Saidi kujaribu kuurukia, bado aliambulia patupu.

Baada ya bao hilo Jamhuri walionekana kutulia na kufanya shambulizi la kushtukiza lililopelekea Mshambuliaji Mwalimu Khalfan aisawazishie timu hiyo.

Hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 huku Jamhuri wakiwa wametawala zaidi mchezo na kuwa wamepiga pasi nyingi zaidi zilizowafikia walengwa.

Dakika ya 53, kazi nzuri ya Mwalimu ilimaliziwa vema na Ammy Bangaseka aliyeukwamisha mpira wavuni na kuiandikia Jamhuri bao la pili. Kuona hivyo, kocha wa Simba, Dylan Kerr aliamua kuwapumzisha Kimwaga, Mussa Mgosi na Said Issa huku nafasi zao zikichukuliwa na Mwinyi Kazimoto, Danny Lyanga na Emery Nimuboma, mabadiliko ambayo yalizaa matunda baada ya Awadhi kwa mara nyingne kuipatia Simba bao la kusawazisha.

Baada ya hapo Kerr aliongeza nguvu kwa kuwaingiza Ibrahim Ajibu na Hamis Kiiza ambao waliliweka lango la Jamhuri katika wakati mgumu ingawa umakini wa Walinzi wao uliwafanya washambuliaji hao wa Simba washindwe kuleta madhara.

Hadi mwamuzi Rashid Farhan anapuliza kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo, timu hizo ziligawana pointi moja kila moja.

Post a Comment

 
Top