BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Akram Msangi, Zanzibar
WATOZA ushuru wa Uganda, URA, leo wametawazwa kuwa mabingwa wapya wa Kombe la Mapinduzi baada ya kuifunga Mtibwa ya Turiani mabao 3-1 latika uwanja wa Amaan mjini Zanzibar.Mtibwa ndio walianza kufanya shambulizi katika lango la URA  kabla Waganda hao hawajatulia na kuanza kutafuta bao ambapo walifanikiwa katika dakika ya 16 baada ya Julius Ntambi kuukwamisha mpira wavuni kwa kichwa.

Baada ya bao hilo mchezo ulionyesha kutulia huku kila timu ikionyesha kusaka bao ingawa Mtibwa walitawala zaidi mchezo hadi mapumziko.

Kipindi cha pili kilianza kwa kosa kosa kadhaa langoni mwa URA lakini uimara wa walinzi na kipa Brian Bwete uliwafanya Mtibwa wasiambulie chochote.Mshambuliaji Peter Lwassa aliyeingia akitokea benchi aliwavuruga Mtibwa kwa mabao mawili ya haraka haraka ya dakika ya 85 na 87 kabla Jaffar Salum hajaipatia Mtibwa bao la kufutia machozi katika dakika ya 90 kufuatia makosa ya kipa Bwete aliyejaribu kumpiga chenga mshambuliaji huyo.

Michuano hiyo imemalizika kwa mabingwa hao kujinyakulia kitita cha sh 10 milioni pamoja na kombe huku Mtibwa wakiambulia sh 5 milioni. Lwassa ameibuka mfungaji bora kwa kuweka nyavuni mabao matatu. Bao jingine alilifunga akiisawazishia URA katika mchezo wa nusu fainali  dhidi ya Yanga

Post a Comment

 
Top