BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
AZAM FC imetolewa kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi inayofanyika visiwani Zanzibar baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Mafunzo, matokeo ambayo yamepelekea baadhi ya nyota wa kikosi hicho kukiri kucheza chini ya kiwango na kuomba radhi.

Miongoni mwa wachezaji waliomba radhi ni Nahodha, John Bocco na Himid Mao ambao ni miongoni mwa wachezaji waanzilishi wa timu hiyo yenye maskani yake Chamazi jijini Dar es Salaam.


Bocco na Mao wameandika ujumbe kwenye mitandao ya kijamii wakielezea hisia zao kwa uchungu wa kutolewa kwenye michuano hiyo na kukiri kucheza chini ya kiwango hata mechi mbili za mwisho za Ligi Kuu kabla ya kwenda kwenye mashindano hayo.

''Napenda kuchukuwa nafasi hii kuwaomba radhi mashabiki wote wa Azam kwa perfomance yetu mbaya tuliyoonyesha kwenye mashindao ya Mapinduzi na mechi mbili za ligi kabla ya kuja huku, matokeo ni sehemu ya mchezo inakubalika lakini kitu kinachoangaliwa ni unapataje matokeo yawe mazuri au mabaya.

''Tumepata matokeo mabaya kutoka kwenye perfomance mbaya zaidi sijawahi kuiona katika timu yetu tangu nilipoanza kucheza hadi hivi sasa hivyo tunawaomba radhi mashabiki wetu wote na kuwaahidi tutajituma na kupigania klabu yetu kwa moyo wetu wote,'' alisema Bocco

Kwa upande wa Mao naye alijutia ubovu wa kiwango chao na kuongeza kuwa anaona aibu kwa kiwango hicho walichokionyesha mechi mbili za mwisho za ligi pamoja na mashindano hayo.

Mechi za mwisho za ligi kuu Azam walishinda bao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar huku wakiifunga tena Mtibwa Sugar bao 1-0, mechi ambazo matokeo yake yamekuwa yakilalamika hasa ya Mtibwa Sugar na kwamba timu hiyo inabebwa.

Katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi, Azam walitoka sare na Mtibwa Sugar ya bao 1-1 na leo wamefungwa bao 2-1 dhidi ya Mafunzo.

Post a Comment

 
Top