BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
MAISHA ya binadamu yanaweza kubadilika ndani ya sekunde moja yakawa mabaya ama mazuri. Hivi ndivyo ilivyo kwa wachezaji wa Stand United ya Shinyanga baada ya jana Mkuu wa Mkoa huo Ally Lufuga kufuata agizo la Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye la timu kukabidhiwa kwa viongozi halali chini ya Mwenyekiti Vincent Amani leo wachezaji wamehamia kula kwa mama ntilie.


Mpaka sasa ni wachezaji 14 pekee ambao wapo kambini na wamekosa huduma ya kupelekewa chakula kama ilivyokuwa hapo awali na hivyo kulazimika kwenda kula kwa mama ntilie kuanzia chai, chakula cha mchana na usiku huu.

Ugumu wa maisha pia uliwakumba wakati wa kwenda mazoezini baada ya kukosa usafiri kwani kambi yao ipo mbali na uwanja wa Kambarage wanaoutumia kama uwanja wao wa nyumbani.

Hii ilitokana na uamuzi uliotolewa kwenye kikao cha jana chini ya mkuu wa Mkoa huyo na kuwaondoa baadhi ya wajumbe walioteuliwa kati ya wajumbe sita waliokuwa wanasimamia timu. Kamati hiyo pia Mwenyekiti wake alikuwa ni Amani ambaye jana hakutokea kwenye kikao hicho alipotakiwa kukabidhiwa timu.

Nahodha wa timu hiyo Jacob Massawe alisema kuwa kwa muda mfupi tu wamejikuta wakiathirika kwa kiasi kikubwa hasa mgogoro huo unapojitokeza wakati wapo kwenye mechi za Ligi Kuu Bara.

''Mpaka muda huu hakuna kinachoendelea, tuna mechi ngumu mbele yetu lakini hakuna wachezaji kambini waliopo hawawezi kucheza nafasi zote hivyo tunaoumia ni sisi, waliopo kambini hakuna anayewaletea chakula kama ilivyokuwa hapo awali.

''Leo nimelazimika kuwapeleka kwa mama mmoja huwa anapika chakula ndiko walikokula, kambi yetu ipo mbali na uwanja hivyo inatuathiri kwani nimewasiliana na Mwenyekiti lakini hajanipa jibu lolote mpaka muda huu,'' alisema Jacob

Nahodha huyo alisema kocha wao Patrick Leiwig ndiye amekuwa akiwapa faraja na kuwajenga kisaikolojia ingawa imeelezwa kuwa matokeo yoyote ya mechi ijayo wapo tayari kuyapokea japokuwa kwa asilimia kubwa yatakuwa mabaya kutokana na maandalizi yao kuwa mabovu.

Post a Comment

 
Top