BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
TIMU za Yanga na Azam zimeshindwa kutambiana leo katika mchezo wa hatua ya makundi uliozikutanisha timu hizo katika dimba la Amaan mjini Zanzibar, hii ni kutokana na kumaliza dakika 90 kwa sare ya bao 1-1.

Kipindi cha kwanza cha mchezo huo uliokuwa wa kukamiana na undava mwingi ilishuhudiwa kikimalizika kwa timu hizo kwenda mapumziko zikiwa hazijafanikiwa kupata bao lolote huku Yanga wakiwa wamemiliki zaidi mchezo.


Kipindi cha pili kilianza kwa Kocha wa Azam, Stewart Hall kumtoa Ame Ali na kumuingiza kiungo Mudathir Yahaya, mabadiliko ambayo yalizaa matunda ambapo dakika ya 58 Kipre Tchetche aliipatia Azam bao la kuongoza baada ya kukimbia na mpira umbali mrefu na kuachia shuti kali la chinichini akiwa katikati ya mabeki watatu wa Yanga.

Bao hilo lilimfanya kocha wa Yanga Hans Van Pluijm ampumzishe mlinzi wa kati Pato Ngoja na nafasi yake ikachukuliwa na Vincent Bossou.

Dakika 63 Azam walipata pigo baada ya John Bocco kuzawadiwa kadi nyekundu baada ya kutokea vurugu. Kadi hiypo ilisababisha Hall amtoe Ramadhan Singano 'Messi' na kumuingiza Frank Domayo ili kuiimarisha timu katika eneo la kati huku pia akiwapumzisha Tchetche na Racine Diouf na nafasi zao zikichukuliwa na Didier Kavumbagu na David Mwantika.


Pluijm yeye kwa upande wake aliwapumzisha Hamis Tambwe na Deus Kaseke na kuwaingiza Paul Nonga na Malimi Busungu, mabadiliko ambayo yalizaa matunda kwani katika dakika ya 83, mpira uliopigwa na Bossou uliokolewa na mlinzi wa Azam lakini akiwa ndani hivyo mwamuzi Mfaume Ally Nassor kuamuru mpira uwekwe kati kuashiria kuwa ni bao halali.

Hadi dakika 90 za mchezo huo zinamalizika Yanga walipata bao moja huku Azam pia wakimaliza na bao lao moja.

Post a Comment

 
Top