BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
MABINGWA wa kutandaza kabumbu Tanzania Bara, Yanga leo wameanza vema michuano ya kuwania Kombe la Mapinduzi baada ya kuisambaratisha Mafunzo mabao 3-0 katika mchezo uliopigwa kwenye dimba la Amaan visiwani Zanzibar.

Mafunzo ndio waliokuwa wa kwanza kulifikia lango la Yanga ambapo katika dakika ya kwanza tu ya mchezo, mlinda mlango wa Yanga, Deo Munishi 'Dida' aliokoa bao la wazi kufuatia shambulizi la kushtukiza lililofanywa na washambuliaji wa Mafunzo.

Baada ya hapo Yanga walianza kulishambulia lango la Mafunzo ambapo mshambuliaji asiye na bahati na michuano hiyo, Amissi Tambwe alipoteza nafasi mbili za wazi ambazo zingeweza kuipatia timu yake mabao kwenye dakika za mwanzo.

Donald Ngoma kushoto

Dakika ya 31, Donald Ngoma aliiandikia Yanga bao la kwanza kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na kiungo Thaban Kamusoko aliyepiga krosi safi ya chini chini na kumkuta mfungaji akiwa peke yake na kuukwamisha mpira huo wavuni.

Kamusoko ambaye alionekana kuwa nyota wa mchezo huo alikimbia na mpira katikati ya uwanja na kumpasia Ngoma ambaye bila ajizi aliiandikia Yanga bao la pili ikiwa ni dakika ya 34.

Katika dakika ya 79 ya mchezo huo ambao haukuwa na kadi hata moja ya njano, Mafunzo walipata penati baada ya beki wa Yanga, Kelvin Yondan kumvuta mshambuliaji Shaban Suleiman aliyekuwa anaenda kumsabahi Dida. Penati hiyo iliyopigwa na Salum Kheri iliokolewa kiufundi na Dida.

Paul Nonga

Dakika moja kabla pambano hilo halijamalizika, Paul Nonga aliyeingia kuchukuwa nafasi ya Tambwe dakika  ya 87, aliifungia Yanga bao la tatu baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na kipa Khalid Mahadhi kufuatia shuti la Geofrey Mwashiuya huku walinzi wa Mafunzo wakidhani mshambuliaji huyo wa zamani wa Mbeya City na Mwadui alikuwa ameotea.

Katika mchezo wa pili, Azam FC watapepetana na Mtibwa Sugar katika uwanja huo huo wa Amaan saa 2:15 usiku wa leo.

Post a Comment

 
Top