BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
TIMU ya Yanga ya jijini Dar es Salaam leo imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ndanda ya Mtwara katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom iliyopigwa Uwanja wa Taifa.Timu zote zilikianza kipindi cha kwanza kwa  kushambuliana kwa zamu huku kiungo wa zamani wa Simba anayekipiga na Ndanda, William Lucian akipoteza nafasi mbili za wazi za kupachika mabao.

Yanga wao wakiwatumia washambuliaji wake wazoefu, Amissi Tambwe na Donald Ngoma waliokuwa wakilishwa mipira na viungo wa pembeni Deus Kaseke na Simon Msuva, walishindwa kuliona lango la Ndanda kutokana umahiri mkubwa wa mlinda mlango Jeremia Kisubi.

Kipindi cha pili Yanga walipata penati baada ya Msuva kuangushwa kwenye eneo la hatari lakini penati hiyo iliyopigwa katika dakika 48 na Tambwe iligonga nguzo na kumrudia ambapo alipiga shuti jingine lililookolewa na mlinda mlango.

Dakika ya 60 Deus Kaseke aliyekuwa akienda kumsabahi Kisubi alikwatuliwa na Braison Raphael na kusababisha penati nyingine safari hii ikipigwa na mlinzi Kelvin Yondan aliyeukwamisha mpira wavuni na kuiandikia Yanga bao pekee.Kocha wa Yanga Hans Van Pluijm aliwapumzisha Tambwe na Kaseke huku nafasi zao zikichukuliwa na Malimi Busungu na Boubacar Issoufou. Kwa upande wa Ndanda, kocha Hamimu Mawazo aliwapumzisha Jackson Nkwera na Braison na kuwaingiza Omega Seme na Masoud Ally.

Kwa ushindi huo Yanga imerejea kileleni ikiwa na pointi 36 sawa na Azam ila inaizidi kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, Simba inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 30

Post a Comment

 
Top