BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
MABINGWA wa kutandaza kabumbu Tanzania Bara, Yanga ya jijini Dar es Salaam leo wamefanikiwa kuongoza kundi B la michuano ya Mapinduzi baada ya kuifunga Mtibwa Sugar mbao 2-1, mchezo huo ulichezwa katika uwanja wa Amaan.

Mtibwa waliwashtua Yanga kwa bao la mapema dakika ya 10 tu ya mchezo lililofungwa na Ramadhan Shiza Kichuya akimalizia pasi nzuri ya Hussein Javu. Baada ya bao hilo Mtibwa waliendelea kutawala mchezo huku wakitengeneza nafasi kadhaa ambazo hazikuzaa matunda.


Dakika ya 42, Issoufou Boubacary aliisawazishia Yanga kwa mpira wa adhabu ndogo ambao aliupiga kiufundi mkubwa na kutinga moja kwa moja wavuni.

Kipindi cha pili kocha wa Yanga, Hans Van Pluijm aliwapumzisha Amissi Tambwe, Donald Ngoma, Boubacary na Thaban Kamusoko huku nafasi zao zikichukuliwa na Malimi Busungu, Paul Nonga, Geofrey Mwashiuya na Salum Telela.

Mabadiliko haya yaliibeba sana Yanga kwavile walianza kutawala mchezo na kufanya mashambulizi kadhaa ya hatari lango mwa Mtibwa ambapo katika dakika ya 81, Busungu aliipatia Yanga bao la ushindi akitumia vema krosi ya Simon Msuva.

Dakika ya 86, mwamuzi wa mchezo huo, Rashid Farhan, alimtoa nje Henry Joseph kwa kadi nyekundu baada ya kucheza rafu mbaya tena akiwa ametoka kufanya madhambi mara mbili  mfululizo. 

Kwa matokeo hayo, Yanga wanamsubiri mshindi wa pili wa kundi A ambalo bado halijatoa taswira ya nani na nani watatinga hatua ya nusu fainali.


Post a Comment

 
Top