BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
CHAMA cha soka Zanzibar (ZFA) kimemtaka Rais wa Shirikisho la soka nchini (TFF), Jamal Malinzi kuomba radha kwa kauli yake ya upotoshaji na kwamba asipofanya hivyo basi watampeleka mahakamani kwa kosa la kutamka kauli ya kibaguzi na uchochezi.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais wa ZFA, Alhaji Ameir Haji aliyeongoza na mwanasheria wa chama hicho, Abdalla h Juma pamoja na wajumbe wa Kamati hiyo ya muda, alisema kuwa Malinzi anawadanganya wananchi wanaopenda maendeleo ya soka kwani yeye alihusika kuunda kamati hiyo anayoipinga na kumtambua Rais wa ZFA, Ravia Idarous Faina.

"Nashangaa sana Malinzi kushirikiana kwa karibu mno na Faina ambaye anaandamwa na tuhuma nyingi za ubathirifu wa pesa za ZFA, Malinzi ndiye alikuwa Mwenyekiti wa kikao kile iweje leo atamke kauli ambayo ni ya kibaguzi na uchochezi, katika kikao ZFA tulikubaliana kufuta kesi na tayari zimefutwa kesi zote mahakamani.

"Tunamuomba Malinzi aombe radhi kupitia vyombo vya habari alivyovitumia na akishindwa kufanya hivyo, tutakwenda mahakamani, kwani anataka kuharibu soka kwa faida ya watu wachache,Kamati iliyoundwa ilianza kufanya kazi ndiyo maana ligi inaendelea na ilikuwa kwenye mchakato wa kufanya mambo mengine ikiwemo mkutano mkuu pamoja na uchaguzi kwani muda wa viongozi wa sasa chini ya Faina ulikwisha," alisema Haji.

Mwanasheria wa ZFA, Juma naye alisisitiza kwamba Malinzi amepotosha ukweli wa kamati hiyo ambayo ameikana na kumtambua Faina pekee, "Si kwamba anasikitisha tu bali anapotosha wananchi, ametamka kauli ambayo si ya kimichezo na haipaswi kuzungumza popote kwani ni ya kibaguzi, mambo mengi yanaendela ila tumekuwa tukiyakalia kimya kwasababu ya kuendeleza upendo na amani katika Muungano wetu,".

Post a Comment

 
Top