BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Marco Ngevenga, Mbeya 
KASI ya Kocha Mpya wa Mbeya City, Kinnah Phiri imetulizwa na Azam Fc baada ya timu yake kukubali kichapo cha bao 3- 0 kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa Uwanja  wa Sokoine Jijini Mbeya.

Kipre Tchetche akipongezwa baada ya kuipatia Azam bao la kwanza

Mchezaji Kipre Tchetche ndiye alikuwa wa kwanza kuzifumania nyavu za City dakika ya 41 baada ya kupigwa mpira wa kichwa akiunganisha mpira wa kona uliopigwa na Himid Mao.

Kipindi cha pili timu zote  zilianza kwa kasi ya kushambuliana, lakini John Bocco wa Azam aliiandikia bao la pili dakika ya 64, ambaye alipokea krosi iliyopigwa na Shomari Kapombe na  Farid Mussa akashindiria bao la tatu  dakika ya 85  akimalizia mpira ambao Kipa wa City Juma Kaseja aliutema kisha akazembea kuufuata ndipo Farid ukamkuta mguuni.

Kuanzia dakika ya 30 ya mchezo mvua kubwa ilianza kunyesha jambo lililowafanya wachezaji kushindwa kumudu mpira ipasavyo kutokana na kudondoka ovyo kwa sababu ya utelezi.


Wachezaji wa City walionekana kutulia zaidi kipindi cha kwanza na kufanya mashambulizi mara kwa mara lango la Azam lakini hawakuwa na bahati ya kupata magoli na kipindi cha pili licha ya kuendelea kutulia uwanjani lakini utelezi ulionekana kuwa  kikwaza kwao kutokana na kushindwa kupiga mipira ya maana wakiwa ndani ya 18 ya lango la Azam.

AZAM WABADILI VIATU UWANJANI.

Wakati wa mapumziko Azam walifanya mabadiliko ya jezi, ambapo kipindi cha kwanza walivaa jezi za  zambarau lakini wakati wakiingia kipindi cha pili walivaa jezi nyeupe.

Wachezaji wa Azam wakishangilia moja ya mabao waliyofunga

Wakati mpira ukiendelea kipindi cha pili, gari aina ya Noah iliingia uwanjani hapo ikiwa mwendo kasi huku wakiwamo viongozi wa Azam, ambapo walionekana kushusha begi jeusi ambalo awali halikujulikana lina kitu gani ndani yake, lakini baada ya dakika chache walifungua begi hilo na kuanza kutoa viatu .

Wachezaji wa Azam walianza kubadilishiwa viatu huku mpira ukiendelea  kwa kile kilichoelezwa wachezaji hao walikuwa wakishindwa kumudu mpira uwanjani kwa sababu ya aina ya viatu walivyokuwa wakivitumia kutokuwa rafiki na hali ilivyokuwa.

Beki wa kulia wa Azam, Shomari Kapombe akimtoka Tumba Sued

Kitendo hicho kilionekana kuwasaidia wachezaji wa Azam kwani walionekana kuanza kumudu mpira huku ile hali ya kudondoka hovyo hovyo haikuwepo bali kazi kubwa ilikuwa kwa wachezaji wa City.

Post a Comment

 
Top