BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Zainabu Rajabu, Dar
Canavaro, aliyesimama katikati akiwa benchi dakika chache kabla pambano la Yanga na Simba halijamalizika

NAHODHA wa Yanga, Nadir Haroub 'Canavaro' ameanza mdogo mdogo baada ya kukaa nje kwa zaidi ya miezi miwili na ametamka kuwa anatamani kurejea kwenye kikosi cha kwanza.

Mechi ya kwanza kucheza tangu aumie ni mechi yao ya Kombe la FA Walipocheza na Mlale JKT na kupata ushindi wa bao 2-1, ushindi ambao uliwapeleka Yanga hatua ya robo fainali. Mechi hiyo ilichezwa siku ya Jumatano, Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.


Akizungumza na BOIPLUS, Canavaro alisema kuwa anaamini atakuwa fiti ila suala la uwepo wake kwenye kikosi cha kwanza anamuachia kocha Hans Pluijm ambaye ndiye mwenye kuamua ingawa hofu yake kubwa ni kupoteza namba kwenye kikosi hicho.


Hofu ya Canavaro imetokana na uwezo aliouonyesha Mtogo Vicent Bossou na kupata ushirikiano mzuri kutoka kwa Kelvin Yondani.


"Sihofii sana ushindani uliopo kwenye safu yetu ya ulinzi ingawa ni mkubwa sana, naamini nidhamu, juhudi na uwezo wangu kwa pamoja ndiyo siri itakayonirejesha kwenye kikosi cha kwanza," alisema Canavaro


Canavaro aliumia Novemba mwaka jana akiwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kikiwa kwenye mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Algeria ambapo Stars ilifungwa bao 7-0.

Post a Comment

 
Top