BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Kombo Ally, Zanzibar
KAMPUNI  ya Ocean Group of Hotel  ya Zanzibar imeamua kuzinunua tiketi zote za kuingilia kwenye mechi za Kombe la Shirikisho na Klabu Bingwa Afrika zitakazopigwa hapa visiwani Zanzibar kwenye dimba la Amani zikihusisha timu za Mafunzo na JKU.

Jacob Makundi alimkabidhi Kahami Ali Machenga wa Mafunzo vitabu vya tiketi za mchezo huo

Mafunzo itajitupa dimbani Febuari 13 kucheza na As Vita ya DRC  ikiwa ni mchezo wa klabu bingwa  wakati JKU wao watashuka dimbani Febuari 14 kupepetana  na vijana wa Gaborone  United kwenye mchezo wa kombe la Shirikisho.

Mbali na kununua tiketi zote za mechi hizo, kampuni hiyo pia imeahidi kutoa shilingi milioni tano kwa kila timu ambayo itaibuka na ushindi katika mchezo wake.

Akizungumza na waandishi wa habari leo hii majira ya saa nne za asubuhi kwenye hoteli yao iliopo Migombani Meneja wa kampuni hiyo Jackob Makundi alisema kuwa kampuni yao imevutiwa  na kutambua umuhimu wa michezo ndio sababu ya kujitolea kufanya hivyo ili wananchi waweze kuiona michezo hiyo.

Meneja huyo alisema kuwa kampuni yao imedhamini kwa kununua tiketi 10,000 za kuingilia uwanjani zenye thamani ya shilingi milioni 10 ambazo zitatolewa bure siku ya mechi kwa kila atakaye fika uwanjani.

"Tutanunua tiketi zote na kuzigawa bure, lakini pia kampuni itatoa fulana kwa viongozi na wachezaji wa timu hizo, pamoja na kutoa punguzo la asilimia 75 ya gharama za malazi kwa viongozi na waamuzi watakaochezesha mchezo huo." alisema Makundi


Kwa upande wake mwanasheria Abdalla Juma kwa niaba ya Mkurugenzi wa kampuni hiyo Amani Ibrahim Makungu, alisema kuwa jitihada zao katika michezo hii ya awali ndizo  zitakazoweza kutoa fursa kwa kampuni yao kuangalia namna ya kuwasaidia katika michezo yao ya marudiano.

Akizungumza kwa niaba ya timu hizo Meja Khamis Mohammed ambaye ni mkuu wa idara ya michezo na utamaduni JKU, alisema kuwa wanakwenda katika kupambambana hivyo amewataka washabiki na wapenda soka Zanzibar kuja kwa wingi Amaan kuwaunga mkono.

"Tunashukuru viongozi wa kampuni hii kwa msaada wao mkubwa ambao wameutoa katika mechi hizo, kwani utaweza kutujenga vizuri kisaikolojia na hatimae kushinda mechi zote tukianzia na hii ya nyumbani. Mashabiki wajitokeze kwa wingi kutuunga mkono ili tufanikiwe." alimaliza Meja Khamis

Post a Comment

 
Top