BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Mwandishi Wetu, Shinyanga
KIUNGO wa Simba, Mwinyi Kazimoto leo asubuhi alifikishwa mahakama ya wilaya ya Shinyanga kujibu tuhuma za kumshambulia Mwandishi wa Habari wa Kampuni ya Mwananchi Communication Limited, Mwanahiba Richard anayeandikia gazeti la Mwanaspoti.


Mwinyi amefunguliwa mashitaka ya shambulizi la kudhuru mwili ambalo anadaiwa kulifanya Februari 10 mwaka huu baada ya mazoezi ya timu yao yaliyofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga.

Mashitaka hayo yalisomwa na mwanasheria wa serikali Upendo Shemkole mbele ya Hakimu Mkazi wa Mkoa, Rahim Mushi ambapo mtuhumiwa alikana kutenda kosa hilo na kuomba apewe muda wa kutafuta wakili wa kumtetea ambapo kesi hiyo imeahirishwa mpaka Machi 21 mwaka huu.

Mwinyi pia atatakiwa kufika na mashahidi wake ambao ni kocha wa Simba, Jackson Mayanja, Yasin Gembe, Abbas Ally ambaye ni Meneja wa timu hiyo pamoja na mtunza vifaa wao Hamisi Mtambo ambao leo hawakufika wakati upande wa mlalamikaji mashahidi wa Mwanahiba ni yeye mwenyewe na Ben Karama pamoja na F1732 koplo Gisibo ambaye alifanya upelelezi wa kesi hiyo.

Baada ya hakimu Mushi kuahirisha kesi hiyo Mwinyi alitakiwa kuwekewa dhamana ya Sh 500,000 na mtu ambaye ni mkazi wa Shinyanga ambayo alitolewa hapo hapo.

Post a Comment

 
Top