BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
TIMU ya soka ya KRC Genk anayoichezea mtanzania Mbwana Samatta, jana imeibuka na ushindi mnono wa mabao 6-1 dhidi ya Waasland-Beveren katika mchezo wa ligi kuu ya Ubelgiji almaarufu Belgium Pro League.Genk waliwatangulia Waasland kwa bao la dakika ya tisa likifungwa na Nikos Karelis kabla wageni hawajasawazisha kupitia kwa Zinho Gano katika dakika ya 18.

Mvua ya mabao ilianza kuwashukia Waasland kwa mabao mengine matatu kwenye kipindi cha kwanza yakifungwa na Kebano, Leon Bailey na Karelis katika dakika za 26, 27 na 31.

Kipindi cha pili Thomas Buffel na Kabasele walihitimisha karamu ya mabao kwa kutupia nyavuni katika dakika za 72 na 84.

Samatta aliingia katika dakika ya 77 akichukua nafasi ya mfungaji wa mabao mawili, Karelis huku akionyesha kuendelea kuelewana vema na wenzake jambo ambalo linatoa matumaini ya kuanza kuisaidia timu yake.

Kwa ushindi huo Genk wamebaki katika nafasi yao ya tano wakiwa na pointi 41 huku Gent wakiongoza kwa point 55 na Club Brugge wakifuatia kwa kujikusanyia pointi 51 na mchezo mmoja mkononi.

Post a Comment

 
Top