BOIPLUS SPORTS BLOG

Imeandaliwa Na Karim Boimanda na Samuel Samuel, Dar

MECHI ya Simba na Yanga haijawahi kuwa ndogo tangu kuanzishwa kwa timu hizo, hawa ni Watani wa jadi na msisimko wa mechi yao huwakumba hata wasiopenda mpira wa miguu. Mwaka huu mchezo wa kwanza utakaozikutanisha timu hizo utapigwa siku ya jumamosi Februari 20 katika uwanja mkuu wa Taifa jijini Dar es Salaam. BOIPLUS inakuletea uchambuzi wa vikosi vyao kuelekea pambano hilo na leo tutaanza na safu ya ulinzi.


 YANGA
Kwa misimu kadhaa safu ya ulinzi ya Yanga imekuwa tishio kwa timu mbali mbali kutokana na uimara wake na hii ilitokana na wachezaji wa nafasi hiyo kudumu kwa pamoja kikosini hapo na kucheza kwa viwango vyao kwa muda mrefu.
Kelvin Yondani moja ya mabeki bora wa kati nchini alijenga ukuta imara na mkoba Nadir Haroub 'Canavaro' nahodha wa timu hiyo ambaye kwa sasa ndie mchezaji mkongwe zaidi kwenye kikosi hicho baada ya kudumu kwa zaidi ya miaka 9.

Mara nyingi Canavaro amekuwa akisimama kama beki namba nne lakini akicheza kama 'sweeper' kikwetu tukimuita Mzee wa kuosha huku Yondani yeye akicheza kama 'Ribelo' wa timu hiyo.
Walinzi wa pembeni kushoto ni Oscar Joshua na ingizo jipya Mwinyi Haji wakati upande wa kulia ni Juma Abdul na baadhi ya mechi kiraka Mbuyu Twite akipewa jukumu hilo. Ali Mustafa 'Barthez' na Deogratius Munishi 'Dida' wamekuwa wakipeana zamu kulinda milingoti mitatu ya lango la vijana hao wa Jangwani.
Safu hii ya ulinzi pia ina Vicente Bossou raia wa Togo na mzawa Pato Ngonyani wote wakiwa walinzi wa kati.UBORA
Katika mchezo huo, eneo ambalo Yanga wanaweza kupata shida ni katika ulinzi. Jambo pekee litakalowaokoa Yanga ni kurejea kwa nahodha wao Canavaro ambaye sifa yake kuu ni kucheza kwa jihad. Bidii yake na moyo wa kujitolea vitawabeba sana wanajangwani hao.


Canavaro ana uzoefu mkubwa na mechi hizi za watani, hatokuwa na presha sana hasa kwavile atakabiliana na washambuliaji ambao ameshakutananao mara kadhaa kama Hamis Kiiza, Ibrahim Ajib na Mussa Hassan 'Mgosi' pamoja na wengine ambao si wazoefu wa mechi hizo kama Hija Ugando na Danny Lyanga.

Kipaji kikubwa cha beki wa kushoto Mwinyi Haji ni faida nyingine kwa Yanga. Beki huyu wa kushoto licha ya uwezo wake mkubwa wa kukaba, amekuwa hatari kwenye kuanzisha mashambulizi na ubora wa krosi zake umeshazidhuru timu kadhaa za ligi kuu.


UDHAIFU
Kwa takribani mwezi mmoja na nusu beki wa kati mahiri Canavaro amekuwa nje ya kikosi hicho baada ya kuumia mguu akiwa na timu ya taifa, sanjari na yeye, beki wa kushoto Mwinyi naye amekosa takribani mechi tatu kwa majeraha ya mguu.

Hii ina maana gani?! Kama mwalimu wa timu hiyo Hans Van Pluijm atawapanga wachezaji hawa bora ila ambao wamekosa mechi za mashindano kwa kipindi kirefu, ufanisi wao hautakuwa kama mwanzo na hii huenda ikawa ni mtaji mkubwa kwa Simba kutengeneza presha muda wote kwa safu hiyo. Kukosa utimamu wa mwili kwa ajili ya mechi 'match fitness' na kuogopa kujitonesha kutawanyima fursa walinzi hao kuitumikia nafasi hiyo kwa asilimia 100.


Lakini pia Yanga itamkosa Yondani ambaye atakuwa anatumikia adhabu ya kukosa mechi tatu kufuatia kadi nyekundu aliyopata katika mchezo dhidi ya Coastal Union. Hii itamlazimu Pluijm kuunda safu ya ulinzi nyingine tofauti na ile iliyozoeleka inayoongozwa na Canavaro na Yondani. 
Kuna uwezekano mkubwa akaamua kuwatumia Canavaro na Bossou katikati ili amtumie Twite kama mlinzi wa kulia baada ya Juma Abdul kuumia katika mechi ya klabu bingwa Afrika dhidi ya Cercle de Joachim huko Mauritius . Zaidi ya hapo Mholanzi huyo hatokuwa na chaguo jingine.

Kwa ujumla safu ya Yanga haitokuwa katika ubora wake uliozoeleka kwavile itakabiliwa na mambo makubwa mawili ambayo ni kuwa na wachezaji wawili waliotoka majeruhi pamoja na kutumia muunganiko 'combination' mpya tofauti na ile iliyozoeana kwa kipindi kirefu.

NINI CHA KUFANYA
Pluijm anajua wanachama na wapenzi wa Yanga hawataki kusikia hizi stori, wanataka ushindi tu ili maisha yao yawe mazuri hapa mjini. Mtaalamu huyo pia anajua kuna udhaifu katika safu yake ya ulinzi, kitu pekee anachoweza kufanya ni kuimarisha eneo la kiungo hasa kwenye ukabaji. Licha ya ubora wa Thaban Kamusoko, kocha huyo atalazimika kumuongezea mtu mwingine atakayepewa jukumu la kukaba ili wawe wawili 'double holding midfielders'. 

Mtu ambaye angefaa zaidi hapa ni Salum Telela ambaye hatokuwepo kwavile ana kadi tatu za njano. Badala yake, Haruna Niyonzima atalazimika kuacha kucheza na jukwaa ili awe msaada mzuri kwa Kamusoko. Viungo wawili wa ukabaji ndio suluhisho pekee kwavile hawa watapunguza uwezekano wa washambuliaji wa Simba kuwafikia mabeki wa timu hiyo mara kwa mara.


SIMBA
Ukali wa safu ya ushambuliaji ya Yanga inayoongozwa na washambuliaji wa kati Donald Ngoma na Amissi Tambwe ambao mara nyingi wanalishwa mipira na viungo wa pembeni Simon Msuva na Deus Kaseke, ni tatizo kwa Simba, hili linafahamika na bila shaka kocha Jackson Mayanja anaumiza kichwa kuona anauzima vipi moto wao. Waandishi wa BOIPLUS wanaelezea ubora na udhaifu wa safu hiyo nyeti.


UBORA
Tangu kutua kwa kocha Mayanja, Simba imecheza mechi saba za kimashindano huku wakifungwa mabao mawili tu. Hii inamaana kuwa wana wastani wa kufungwa bao moja kila baada ya dakika 315 ambazo ni zaidi ya masaa matano mfululizo ya kucheza mpira. Wazungu wanasema "Men lie, women lie but number don't lie". Hapa  ni wazi safu ya ulinzi ya Simba iko vizuri, namba hazidanganyi.

Muunganiko wa Juuko Murshid na Hassan Isihaka umekuwa bora zaidi huku wakijivunia viungo wawili wakabaji Jonas Mkude na Justice Majabvi ambao wamesababisha mabeki hawa wapate majaribu machache. Upande wa kuliaMayanja akiamua kumtumia Emery Nimubona au Hassan Kessy bado moto ni ule ule kwavile wote ni wazuri kwenye kupokonya mipira na kuanzisha mashambulizi. Kushoto Abdi Banda anaweza kuziba vema pengo la Mohamed Hussein 'Tshabalala' ambaye licha ya kuanza mazoezi akitokea majeruhi, bado atakosa utimamu wa mwili.

UDHAIFU
Isihaka ni beki anayefanana mambo mengi sana Canavaro wa Yanga, wanacheza kwa jihad, wanatumia nguvu na hawapendi sifa.....wao wanaosha tu hakuna kuremba, tatizo lao ni makosa 'hatarishi' kwenye eneo la hatari. Isihaka anaweza kufanya kosa ambalo likasababisha uwanja mzima watu waweke mikono kichwani. Ukiwa na mshambuliaji makini na mviziaji maarufu kama Tambwe hupaswi kukosea, huruhusiwi kabisa, na ukijaribu atakupeleka nyavuni ukaokote mpira. 

Hapa Simba wanaweza kushtuka wanatafuta mchawi baada ya kufanikiwa kuondosha hatari nyingi ambazo ni ngumu halafu waje kufungwa bao kwa shambulizi la kawaida sana. Na inafahamika matokeo ya mechi hizi hayategemeani sana na ubora wa timu, bali nani katumia vema nafasi hata moja tu aliyoipata.


Jambo jingine ambalo Simba watapaswa kuwa makini nalo ni aina ya uchezaji wa Juuko. Mechi za watani zina mambo mengi, migongano baina ya wachezaji na rafu za makusudi ni kawaida sana. Beki huyu anayesifika kwa kuweka 'sura ya mbuzi' anapaswa kuwa makini sana ili kuepuka kadi. Waamuzi wamemkariri kuwa ni beki mkorofi, hii ni mbaya kwavile uwezekano wa kupata kadi nyekundu ni mkubwa. Ikitokea hivyo itaidhoofisha Simba kwa kiasi kikubwa.

NINI CHA KUFANYA
Isihaka ameshacheza mechi nyingi za watani sasa, anapaswa kuonyesha ukomavu, atulie na kuepuka makosa ya 'kitoto'. Lakini pia itabidi Juuko awe 'Bwana Usafi' wa kuhakikisha mahala pa Isihaka hapana uchafu wowote, wakati wote awe jirani yake kuhakikisha anasafisha kila kosa atakalolifanya. 

Jambo jingine Juuko mwenyewe awe makini kwenye kila atakachofanya na acheze kwa kuepuka kadi, vinginevyo anaweza kuwa sababu ya matokeo mabaya kwa Simba.

Usikose kusoma makala ya pili itakayozungumzia ubora na udhaifu wa timu hizo katika idara ya Kiungo na Ushambuliaji

Kwa maoni;
Simu; +255788334467 

Post a Comment

 
Top