BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda, Dar
MTOTO hatumwi dukani, na ukimuona dukani ujue kaenda kununua pipi yake. Lakini pia waswahili husema "Ukitaka kumfukuza paka nyumbani, we acha kupika." Ule ubishi wa kipindi kirefu unamalizwa masaa machache tu yajayo katika dimba la Taifa jijini Dar es Salaam pale watani Simba na Yanga watakapopepetana.


Picha kwa hisani ya SOKA360

BOIPLUS ilianza kuzichambua safu za ulinzi na kiungo za timu hizo, na leo tunamaliza kwa kuzidadavua safu za ushambuliaji. 

YANGA
Ukikataa we mbishi, hadi kabla ya mchezo wa leo, safu ya ushambuliaji ya Yanga ndio imefunga mabao mengi zaidi ikiwa  imepachika nyavuni mabao 42. Unataka nini zaidi kusema hii mdio safu kali zaidi ya ushambuliaji?. Namba hazidanganyi bwana.

'Combination' ya Amiss Tambwe na Donald Ngoma peke yake imeshazamisha mabao 24 nyavuni. Wakali hawa wanatiwa kiburi na mawinga teleza Simon Msuva na Deus Kaseke ambao wamehusika katika utengenezaji wa mabao mengi sana ya Yanga. Kuwatoa uwanja wa Taifa bila bao ni kazi ngumu sana ambayo ikikamilika itabidi tuwavishe nyota mabeki wa Simba.Tambwe 'The Silent Killer' ambaye mimi naamini ndiye mviziaji bora kabisa kwasasa hapa nchini, ni mchezaji ambaye mara nyingi amekuwa mgumu kumfanyia 'marking'. Hana makeke na hatumii nguvu nyingi, si rahisi kumfikiria muda wote, na pale utakapomsahau ndipo utakapomuona akishangilia.

Kocha wa Yanga Han Van Pluijm atampa Ngoma kazi ya kupambana na akina Juuko Murshid ili Tambwe abaki huru. Lakini pia Thaban Kamusoko ni hatari kwa mipira mirefu, anatumika kuanzisha mashambulizi kwa kutupa mipira kwa mawinga lakini kuna wakati rasta zake 'zikimuwasha' huamua kunyoosha goti. Vicent Angban ni lazima awe makini na mipira hii ya kushtukiza, vinginevyo atalazimika kwenda kuokota mpira nyavuni.

Baada ya dakika tisini turudi kusoma tena hii makala.SIMBA
Ningekuwa naiongelea Simba ya Dylan Kerr, wala nisingepata shida. Haikuwa na morali kama hii ya Jackson Mayanja. Ningesema tu tusubiri kudra za MUNGU kupata matokeo. Lakini kwa hii ya Mayanja lazima nisema kitu.

Safu ya Simba haijafunga mabao mengi kuifikia ile ya Yanga, lakini tangu mganda huyo aanze kuinoa, wapinzani wao wamekuwa kwenye wakati mgumu sana. Katika mechi saba tu alizoiongoza, Simba imefunga mabao 18 huku mganda mwenzake Kiiza akiwa ameshatupia 'kunyavu' mara 16 tangu ligi ianze na kuwa kinara wa mabao.Mahusiano kati ya kiungo na washambuliaji wa Simba yameimarika sana, jana niliwashauri Yanga kuwa kama wanataka kuizima safu ya ushambuliaji ya Simba basi wakate 'waya' wa mawasiliano kati ya Mwinyi Kazimoto na mastraika wa timu hiyo.

Kasi ya ufungaji ya Kiiza katika viwanja vyote (vibovu na vizuri) inatisha, Yanga ni lazima wakubali hilo ili waweze kumzuia. "Kukubali ubora wa adui yako ni hatua ya kwanza ya kumshinda."
Kiiza anapewa kiburi na viungo wa timu hiyo huku huyu kijana anayeaminika kuwa 'fundi' zaidi kwasasa, Ibrahim Ajib amekuwa mtu hatari sana, anajua kufunga mabao lakini si mroho. Na hii ndio sababu anapendwa sana na Kiiza, si anampikia 'chakula' cha kutosha bwana.

Tuongee uhalisia, kuwatoa Kiiza, Ajib, Danny Lyanga, Hija Ugando, Mussa Mgosi na Mwinyi Kazimoto bila bao pale taifa ni kazi ngumu ambayo ikifanikiwa nitasema "shikamoo mabeki wa Yanga."

Msomaji wetu usikose kutembelea kurasa zetu za Facebook, Instagram na Twitter (BOIPLUS BLOGSPOT) ili kuona video za kila kinachojiri kuanzia mitaani hadi uwanja wa Taifa.

Kwa maoni:

E-mail; boiplus.blogspot@boi.co.tz
Mobile; +255788334467

Post a Comment

 
Top