BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
LICHA ya kutawala mchezo kwa kiasi kikubwa, Manchester City wamechezea kichapo cha mabao 3-1 kwenye uwanja wao wa nyumbani ilipopambana na Leicester City katika mchezo wa ligi kuu nchini Uingereza.


Leicester waliishtukiza Manchester City kwa bao la 'alfajiri' katika dakika ya tatu tu ya mchezo likifungwa na Robert Huth akimalizia mpira wa adhabu ndogo uliochongwa na Riyad Mahrez.

Kipindi cha pili ndipo hali ilipogeuka na kuwa mbaya zaidi kwa Man City kwani katika dakika ya 48 Mahrez aliiandikia Leicester bao la pili kwa shuti kali kabla Huth hajapiga la tatu katika dakika ya 60.

Juhudi za Man City kusawazisha mabao hayo ziliendelea kupunguzwa nguvu na walinzi wa Leicester ambao walitumia mtindo wa 'beki hasifiwi' kwa kuosha kila hatari iliyoelekezwa langoni mwao.

Sergio Aguero aliipatia Man City bao la kufutia machozi katika dakika ya 87 kwa kichwa akimalizia krosi ya Bersant Celina.

Kwa matokeo hayo vijana wa Claudio Ranieri wanaendelea kuongoza ligi wakiwa na pointi 53 wakifuatiwa na City ambao wanabaki na pointi zao 47.

Post a Comment

 
Top