BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Zainabu Rajabu, Dar
BEKI wa Simba, Abdi Banda jana Jumamosi alipewa kadi nyekundu na kulazimika kutoka uwanjani akiiacha timu yake ikipambana na Yanga ikiwa pungufu jambo ambalo limeonekana kutomfurahisha kocha wake, Jackson Mayanja.


Mayanja ametamka kuwa timu yake kucheza pungufu kutokana na kadi hiyo ndiko kulisababisha washindwe kupata mabao huku watani wao wakitumia upungufu huo kuwamaliza na kupata pointi tatu zilizowarudisha kileleni wakati wao wakishuka mpaka nafasi ya tatu.

Mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara ilichezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo Yanga ilishinda bao 2-0 hivyo kufikisha pointi 46 huku Simba ikibaki na pointi 45 sawa na Azam FC ambayo imepanda nafasi ya pili baada ya kuifunga Mbeya City bao 3-0.

Banda alionyeshwa kadi mbili za njano na refa Jonesia Rukyaa kutoka Bukoba ndani ya dakika nne kwa kumchezea rafu Donald Ngoma mara zote na kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 23.

Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Mayanja alisema "Tulicheza vizuri sana dakika 20 za mwanzo, lakini baada ya kadi ilibidi tubadili mfumo na wenzetu wakatumia nafasi hiyo kutushinda najipanga katika mechi zijazo,"

Tangu Mayanja aanze kuifundisha Simba hii ni mechi yake ya kwanza kupoteza huku akiwa ameshinda mechi sita za ligi kuu na moja ya Kombe la Shirikisho.

Post a Comment

 
Top