BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Marco Ngavenga, Mbeya
TIMU ya Prisons ya jijini Mbeya nayo imetinga hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la TFF baada ya kuifunga Mbeya City bao 2-1, mechi hiyo imechezwa Uwanja wa Sokoine.


Benno Kakolanya

Prisons ni timu ya nne kutinga hatua hiyo ikitanguliwa na Yanga, Coastal Union pamoja na Mwadui Fc.

Mohamed Mkopi wa Prisons ndiye aliyeanza kucheka na nyavu za wapinzani wao dakika ya 40 akifunga kwa kichwa baada ya kuunganisha mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Salum Kimenya nje kidogo ya lango la Mbeya City.

Faulo hiyo ilitokana baada ya mchezaji wa Prisons, Jeremiah Juma kufanyiwa madhambi na Haruna Shamte matokeo ambayo yalidumu mpaka kwa kipindi cha kwanza.Dakika ya 47, Mbeya City ilipata bao la kusawazisha lililofungwa na  Joseph Mahundi akiunganisha krosi ya pembeni iliyopigwa na Haruna Moshi  'Boban'.

Hata hivyo, Prisons ilionyesha umwamba wake baada ya kufunga bao la pili dakika ya 82 likifungwa na kipa anayeng'ara zaidi Benno Kakolanya akipiga mpira wa adhabu baada ya mchezaji wa City kuotea. Mpira huo uliopigwa umbali wa takribani mita 70 ulidunda na kumpita kipa wa City Hannington Kasyebula ambaye alikuwa amesogea mbele zaidi.

Mechi hiyo ilikuwa na upinzani mkubwa kutokana na timu zote kuwa za jijini Mbeya ilianza kuchezwa huku mvua kubwa ikinyeesha na wachezaji wa pande zote mbele kushindwa kucheza kwa utulivu kipindi cha kwanza mpaka mvua ilipokatika.


Hali ilivyokuwa uwanjani wakati mvua ikiendelea kunyesha

Mechi nyingine ya kombe la TFF ilikuwa ni kati ya Mwadui FC ya Shinyanga na Rhino Rangers ya Tabora ambapo Mwadui imeshinda mabao 3-1. Mabao ya Mwadui yamefungwa na Jerry Tegete (2) na Rashid Mandawa (1) huku lile la Rhino likifungwa na Edgar Edson.

Post a Comment

 
Top