BOIPLUS SPORTS BLOG

Imeandaliwa Na Karim Boimanda na Samuel Samuel, Dar

YAMEBAKI masaa takribani 26 tu nyasi za uwanja wa Taifa zipate tabu kwa wababe wa soka nchini, watoto wa Kariakoo Simba na Yanga kupepetana kwenye mchezo wa ligi kuu ya Vodacom.

Jana BOIPLUS ilikuletea uchambuzi wa ubora na udhaifu wa safu za ulinzi za timu hizo. Tumepokea maoni mengi kutoka kwa wasomaji wetu wengi sana, tunashukuru sana kwavile inaonyesha mnafuatilia mtandao wetu. Leo tunahamia kwenye eneo la kiungo, twende pamoja.


SIMBA
Msimu uliopita, Simba ilikuwa na viungo wazuri tu lakini ilikosa kitu kimoja, nacho ni viungo wengine wa kukaa benchi ili kutoa msaada pale wale walioanza wanapofeli kwenye kutengeneza mipango ya ushindi. Hali ni tofauti na sasa, ndani wakiwepo Jonas Mkude, Justice Majabvi na Mwinyi Kazimoto, bado nje kunakuwa na viungo wengine mafundi kama Said Ndemla, Awadh Juma na Brian Majwega.

Utajiri huu wa viungo umeleta mafanikio makubwa ndani ya kikosi cha Simba kwavile licha ya kocha Jackson Mayanja kuwa na machaguo mengi, ushindani wa namba umeongezeka na kuwafanya wachezaji kuwa na bidii zaidi ili kuepuka kusugua benchi.

Hakuna shaka Mayanja atawatumia Mkude na Majabvi katika kiungo cha kukaba (holding Midfield) huku Kazimoto akicheza kama kiungo mchezeshaji. Kwa mechi kadhaa Yanga wamekuwa wakipata shida kwenye eneo la kiungo kwavile tu wao mara nyingi hutumia viungo wa kati wawili tu, mmoja akiwa mkabaji na mwingine mshambuliaji. Walipobadilika na kutumia watatu katika mchezo wao uliopita dhidi ya Simba, kila mmoja alishuhudia jinsi eneo la kiungo lilivyokuwa na upinzani mkubwa hadi kupelekea Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Katika mchezo wa kesho inawezekana kabisa Kocha wa Yanga Hans Van Pluijm akaweka tena viungo wawili wakabaji ili kuongeza usalama kwenye safu ya ulinzi ambayo ni dhahiri imepata mushkeri kutokana na kukosekana kwa Kevin Yondan na Nadir Haroub ambaye bado ana hatihati ya kucheza baada ya jana kushindwa kumaliza mazoezi baada ya kupata maumivu.

Kutokana na hili, Simba ina nafasi kubwa ya kutawala eneo la kiungo kwavile viungo wa Yanga wanaweza kuweka nguvu zaidi kwenye kuulinda ukuta wao ambao umeonekana kuwa dhaifu kuliko kuanzisha mashambulizi.Kazimoto amekuwa 'Mcharo' katika mechi takribani saba alizoanza hivi karibuni, ameonyesha uwezo mkubwa katika kukaba, kupokonya mipira, kutoa pasi za mabao na hata kufunga. Na hii ndio sababu mashabiki wa Simba wamekaa kimya na wameacha kupiga kelele kuhusu kipenzi chao Ndemla kukalia benchi. 

Tatizo la Kazimoto ni moja tu, amekuwa akipungua kasi katika dakika za mwisho, hii ni hatari sana kwavile bao hufungwa katika dakika yoyote, Yanga wanaweza kutumia udhaifu huo kupenya na kutawala eneo la kiungo na kupeleka kilio Msimbazi. Hapa Mayanja atalazimika kumuingiza Ndemla mara atakapogundua kasi ya Kazimoto imeanza kupungua.


YANGA
Ukijaribu kuyafikiria majina ya wachezaji wa Yanga wanaoweza kucheza eneo la kiungo, halafu ukawakumbuka wale viungo wa Simba, unaweza kuhitaji dawa ya kutuliza maumivu ya kichwa. Tumeshaona ubora wa Mkude, Majabvi na Kazimoto ambao wanachagizwa na Ajib na Ugando wanaoshambulia wakitokea pembeni, lakini swali ni je, Hans Van Pluijm akichukua watano tu kati ya Mbuyu Twite, Said Juma, Simon Msuva, Deus Kaseke, Thaban Kamusoko, Haruna Niyonzima na Boubacary Issoufou, akawaanzisha katika mechi ya kesho, hali itakuaje?

Ni vita isiyoelezeka, jambo pekee linaloweza kuidhoofisha Yanga katika eneo hili ni udhaifu wa safu ya ulinzi inayohitaji msaada zaidi kutoka safu ya kiungo kama tulivyoeleza hapo awali, si ubora wa viungo wao. Hakuna mashaka yoyote kuwa Yanga ina viungo wengi na bora. Tatizo ni kwamba ukabaji utatakiwa uanzie kwenye eneo la kiungo, hii inaweza kuwafanya wafikirie kulinda zaidi kuliko kushambulia.


Lakini bado Yanga wanaweza kushinda vita hii kama wataendeleza ubora wao katika kupiga mipira mirefu ambayo mara nyingi  imekuwa ya manufaa kwao kwavile kwa miaka yote wamekuwa na bahati ya kuwa na  viungo bora wa pembeni (wings).

Kasi ya viungo wa pembeni Msuva, Kaseke na lhata Niyonzima inaweza kuwa tishio kwa Simba kama tu Yanga wataamua kulisusa eneo la kati na kucheza mtindo wa 'Mkoa kwa Mkoa' . Hii itafana kama Pluijm ataamua kuwapanga  Kamusoko na Makapu (kwavile Telela hatokuwepo) katika kiungo cha chini. Makapu ni mzuri kwenye kukaba ingawa wakati mwingine hupaniki na kucheza rafu za ajabu zinazoweza kumsababishia kupata kadi. Kamusoko yeye ni mzuri sana katika mipira mirefu kwenda kwa viungo wa pembeni, huyu ndiye ambaye anaweza kuidhuru Simba kama hatoangaliwa kwa umakini.

Ili Yanga waimalize Simba inayotumia pasi fupi fupi katika eneo la kiungo ni lazima wahakikishe wanakata waya wa mawasiliano kati ya Kazimoto na washambuliji wa timu hiyo. Kwa wachezaji waliopo Yanga kwa ajili ya mchezo huo, Makapu ndiye anafaa kupewa jukumu hili. Pluijm atapaswa kumjenga kisaikolojia ili awe makini katika matumizi makubwa ya nguvu ambayo mara kadhaa yamemsababishia majeraha na wakati mwingine kadi zisizo za lazima. 

Twite angeweza kufaa hapa lakini ana tatizo kubwa la kushuka sana chini na kujumuika na mabeki, hii inamnyima nafasi ya kupiga pasi kutokea katikati kwa ajili ya kuanzisha mashambulizi.

Simba haiwategemei sana viungo wa pembeni katika kuanzisha mashambuli, bali huwatumia zaidi mabeki wa pembeni (wing backs) Hassan Kessy, Abdi Banda na Emery Nimuboma ambao wapo tayari kwa mchezo wa kesho. Njia pekee ya kuwazuia wasilete madhara ni kuwapa kazi ya kukaba muda wote wasahau kupanda kushambulia. Hili ni jukumu la mawinga wa Yanga, watalazimika kuhakikisha wanawasumbua na kuwapa kazi ya kuwachunga muda wote. Tofauti na hapo, mabeki hawa ni tatizo jingine kwa Yanga.

HITIMISHO
Zico 'The white Pele', mmoja wa magwiji wa soka duniani aliyetamba na kikosi cha Brazil aliwahi kusema "Utimamu wa timu hupimwa kwa ubora wa nafasi ya kiungo." Hakukosea hata kidogo, nafasi ya kiungo peke yake inabeba matokeo ya mchezo kwa zaidi ya asilimia 60.

Kwenye kiungo ndipo inapoanzia mipango yote ya kujilinda na kushambulia. Mwisho wa siku, eneo la kiungo ndilo litakaloamua matokeo ya mchezo huu wa watani wa jadi. 

Usikose sehemu ya mwisho ya makala hii itakayoelezea safu za ushambuliaji za timu hizo

Kwa maoni:
E-mail; boiplus.blogspot@boi.co.tz
Mobile; +255788334467

Post a Comment

 
Top