BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda, Dar
TIMU ya Simba leo imeonyesha gadhabu zake za kufungwa na Yanga mabao 2-0 wiki iliyopita kwa kuishushia mvua ya mabao 5-1 Singida United ya mjini Singida. Mchezo huo wa hatua ya 16 bora ya michuano shirikisho ulichezwa kwenye dimba la Taifa jijini Dar es Salaam.


Simba walianza kupata bao katika dakika ya tatu tu kupitia kwa Danny Lyanga akimalizia mpira uliookolewa na mabeki wa Singida United.

Baada ya bao hili Simba walitengeneza nafasi kadhaa lakini washambuliaji wake hawakuwa makini kumalizia. Dakika ya 19 Hamis Kiiza aliipatia Simba bao la pili akimchambua kipa wa Singida United Jacton Munna kabla kipa huyo hajaokoa shuti kali la Jonas Mkude kwenye dakika ya 40.

Kipindi cha pili Simba waliendeleza karamu ya mabao kwa Kiiza kutupia bao la tatu kwenye dakika ya 65 kabla Awadh Juma hajafunga mabao mawili ya haraka haraka katika dakika za 82 na 86.

Ikionekana kama vile pambano hilo lingeisha kwa Singida United kupigwa mabao 5-0, beki wa kushoto wa timu hiyo alifunga bao zuri la kufutia machozi kwa shuti kali katika dakika ya 90.

Kwa ushindi huo Simba inatinga hatua ya robo fainali ikiungana na Yanga, Coastal union, Ndanda na Mwadui 

Post a Comment

 
Top