BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
LEO katika uwanja ujulikanao kwa jina la Stade dé la Kenya kumepigwa mechi ya kukata na shoka iliyowakutanisha vigogo wa jiji la Lubumbashi, TP Mazembe na FC Lupopo.


Pambano hilo la ligi kuu ambalo hujulikana kama 'Katanga Kibassa Derby' lilimalizika kwa timu hizo kutoka sare ya bila mabao licha ya mashambulizi kadhaa kufanywa.

Mechi hiyo iliingia dosari katika dakika ya 40 pale Polisi walipopiga mabomu ya machozi nje ya uwanja huo ili kuwatawanya mashabiki waliokuwa wakifanya vurugu. Mabomu hayo yaliwafanya wachezaji washindwe kupumua vizuri hivyo mechi hiyo ikasimamishwa kwa dakika 5 ili hewa safi irejee.

Mechi zote zinazohusisha timu hizi huchezwa katika uwanja huo kwavile Rais wa Mazembe, Moise Katumbi aliamua hata mechi za nyumbani wakachezee huko na si kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Stade dé TP Mazembe kwavile kila mechi hiyo inapochezwa hapo mashabiki hufanya vurugu na kuharibu uwanja huo.

Katika dakika 56, mtanzania Thomas Ulimwengu aliipatia Mazembe bao lakini mwamuzi wa mchezo huo alilikataa kwa madai kuwa mfungaji alikuwa ameotea.

Kwa matokeo hayo Mazembe imemaliza ikiwa kinara kwa pointi 42 huku Lupopo wao wakishika nafasi ya tatu kutokana na pointi 37 walizojikusanyia. Timu hizo zote mbili zimefuzu katika hatua inayofuata 'Play - Off'.

Post a Comment

 
Top