BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Akram Msangi, Dar
UONGOZI wa Yanga leo umetangaza kuwa timu hiyo itaondoka siku ya ijumaa Februari 12 majira ya asubuhi kuelekea nchini Mauritius kwa ajili ya mechi ya michuano ya klabu Bingwa Barani Afrika dhidi ya Cercle de Joachim. 


Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi uliopita Mkuu wa kitengo cha habari na mawasiliano wa Yanga Jerry Muro alisema
"Kamati ya mashindano imeona ni busara timu kuondoka ijumaa kwa ndege maalum ya kukodi itakayobeba kikosi kutoka Dar es salaam moja kwa moja mpaka Mauritius na kisha ndege hiyo itasubiri timu mpaka siku ya jumamosi itakapomaliza mechi na kuondoka jumamosi hiyo hiyo usiku na kuelekea kambini kisiwani Pemba ambako itaweka kambi ya kujiandaa na mchezo dhidi ya Simba hapo Februari 20." 

Muro alisema hatua hiyo inalenga kupunguza usumbufu kwa msafara wa timu haswa wachezaji wakati wa kwenda na kurudi kutokana na kubainika kuwa timu ingelazimika kutumia muda mwingi wa zaidi ya masaa nane kusubiria kubadilisha ndege nchini Afrika kusini wakati wa kwenda na kurudi. 


"Hatua hii inalenga kuondoa mianya ya hujuma na pia kuondoa usumbufu wa uchovu kwa wachezaji haswa kipindi hiki ambacho tunajiandaa na mchezo dhidi ya simba."alifafanua Muro

Kutokana na mabadiliko hayo kikosi kitaendelea na kambi ya mazoezi jijini Dar es Salaam mpaka siku ya ijumaa asubuhi wakati ambapo msafara wa timu utaondoka nchini kuelekea Mauriutius. 

Yanga ilikua iondoke leo asubuhi kuelekea Mauritius kabla ya kupangua ratiba yake.

Post a Comment

 
Top