BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda, Dar

TIMU ya Yanga leo imeifunga Cercle de Joachim ya Mauritius mabao 2-0 na kuiondoa kwenye michuano ya klabu bingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-0 .Mechi hiyo imepigwa katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam

Yanga ilikianza kipindi cha kwanza kwa kucheza mpira wa taratibu na uliopooza lakini wakionekana kuwa ni wenye mipango thabiti wakifanya shambulizi kali langoni mwa CDJ katika dakika ya tatu tu ya mchezo ambapo Amissi Tambwe aliipatia timu hiyo bao kwa kichwa.

Baada ya bao hilo Yanga walifanya mashambulizi kadhaa ambayo hayakuzaa matunda huku CDJ wao walikuwa wakicheza vizuri eneo la kati na kuharibu kila wasogeapo langoni mwa Yanga.  

Kipindi cha pili hali iligeuka kuwa mbaya zaidi kwa CDJ baada ya Yanga kuhamishia kambi langoni mwao na kufanya mashambulizi mengi mfululizo. Kama si kukosa umakini kwa washambuliaji wa Yanga basi timu hiyo ya mtaa wa Jangwani ingevuna mabao mengi zaidi.

Dakika ya 55, Thaban Kamusoko ambaye alikuwa nyota wa mchezo huo aliifungia Yanga bao la pili kwa shuti kali akimalizia mpira wa adhabu ndogo uliopigwa kwa mtindo wa pasi.

Baada ya bao hilo Yanga waliendelea kulishambulia lango la CDJ huku Tambwe, Malimi Busungu na Simon Msuva wakipoteza nafasi kadhaa za magoli.

Katika hatua inayofuata Yanga itakabiliana na kati ya Mbabane Swallows au APR ya Rwanda.

Post a Comment

 
Top