BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda, Dar
MABINGWA wa kutandaza kabumbu nchini Tanzania, Yanga ya jijini Dar es Salaam, leo imeibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya JKT Ruvu katika mchezo wa Ligi kuu uliopigwa kwenye uwanja wa Taifa.Simon Msuva alimpeleka Shaban Dihile nyavuni kwa bao la dakika ya 12 kabla Yanga haijatawala mchezo huo kwa kiasi kikubwa na kuiweka roho juu safu ya ulinzi ya Ruvu.

Dakika ya 44, Issoufou Boubacar aliitumia vema pasi ya Simon Msuva na kuiandikia Yanga bao la pili kwa shuti kali la jirani kabisa na lango la Ruvu.

Kipindi cha pili Yanga iliendelea kulishambulia lango la wanajeshi hao hali iliyopelekea Donald Ngoma aipatie timu yake bao la tatu katika dakika 63 akimalizia kwa kichwa krosi ya Juma Abdul kutoka upande wa kulia.Ikionekana kama pambano hilo lingemalizika kwa Yanga kupata ushindi wa mabao 3-0, Msuva alihitimisha karamu ya mabao kwa kupachika bao la nne safari hii akimaliza pasi ya kupenyeza ya Deus Kaseke.

Kwa matokeo hayo Yanga inaendelea kuumana kileleni na Azam iliyoshinda bao 1-0 dhidi ya Mwadui leo, zikiwa na pointi 43 kila moja, Simba iliyoipiga Kagera 1-0 inashika nafasi ya tatu kwa kuweka kibindoni pointi 42

Post a Comment

 
Top