BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda, Dar
HATIMAYE ubishi umemalizika, watoto wa Jangwani Yanga wameibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Simba katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom uliopigwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.


Thaban Kamusoko kushoto, akimpongeza Donald Ngoma baada ya kuifungia Yanga bao la kwanza

Simba ilikianza kipindi cha kwanza kwa kasi wakionekana kuwamudu vilivyo Yanga huku wakifanya mashambulizi kadhaa yasiyo na matunda. 

Hali ilibadilika katika dakika ya 23 baada ya mlinzi wa kati wa Simba Abdi Banda kulimwa kadi ya pili ya njano ikifuatiwa na nyekundu baada ya kumchezea rafu Donald Ngoma. Baada ya hapo Simba ilionekana kuelemewa huku wakicheza kwa kujihami zaidi ikiwaacha Yanga wakitawala eneo la kiungo cha kati ambalo sasa lilibaki na Jonas Mkude na Mwinyi Kazimoto pekee kwani Justice Majabvi alirudi kucheza beki wa kati.

Dakika 39 Donald Ngoma aliwainua vitini mashabiki wa Yanga kwa kupachika nyavuni bao baada ya kumpita kipa Vicent Angban.

Kipindi cha pili kocha wa Simba Jackson Mayanja aliamua kumtoa Kazimoto huku akimuingiza Novaty Lufunga ili kuimarisha ulinzi na kumrejesha Majabvi katika kiungo, hata hivyo Simba hawakueleweka walicheza mtindo gani baada ya mabadiliko hayo.


Ramadhan Kessy akimtoka Simon Msuva baada ya kumpokonya mpira

Mabadiliko hayo hayakuzaa matunda kwani katika dakika ya 79, Amissi Tambwe alipachika bao la pili akimalizia krosi ya Geofrey Mwashiuya aliyeingia badala ya Deus Kaseke.

Baada ya bao hilo Yanga waliendelea kutawala mchezo huku  wakionyesha kujiamini zaidi. Hadi mwamuzi Jonesia Rukya anapuliza kipenga kuashiria kumalizika kwa mchezo huo, Yanga walijizolea pointi tatu.

Kwa ushindi huo Yanga imekamata usukani wa ligi kwa kufikisha alama 46 ikifuatiwa ma Simba yenye alama 45 sawa na Azam iliyoshinda mabao 3-0
Stand United ametoka sare ya bao 1-1 dhidi ya JKT Ruvu wakati mjini Tanga Mgambo imetoka sare ya bao 1-1 na Prisons.


Post a Comment

 
Top