BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Zainabu Rajabu, Dar

KLABU ya Azam FC ya jijini Dar es Salaam imesema ina uhakika wa kusonga mbele kwenye michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika dhidi ya Esperance ya Tunisia baada ya kugundua mbinu zao.

Kikosi hicho kinachonolewa na Muingereza Stewart Hall kitashuka dimbani kumenyana na waarabu hao April 10 kwenye uwanja wa Azam complex Chamazi kikiwa na matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi baada ya kugundua mbinu mbali mbali za kuitoa klabu hiyo yenye historia kubwa barani Afrika.

Akizungumza na BOIPLUS Kocha msaidizi wa Azam, Dennis Kitambi alisema wanawafuatilia kwa karibu wapinzani wao na tayari wameshazijua mbinu wanazotumia kitu ambacho kinawasaidia kujipanga zaidi kuwakabili.


"Tumekuwa tukiwafuatilia wapinzani wetu ili kujua mbinu zao za kiuchezaji na wachezaji wao hatari ili tuwadhibiti kwenye mechi ya hapa nyumbani tushinde na kuweka mazingira mazuri kwenye mechi ya marudiano kwao." alisema Kitambi.


Kwa upande mwingine nahodha wa timu hiyo John Bocco 'Adebayor' alisema wanaiheshimu timu hiyo kutokana na historia yake barani Afrika lakini hawatishiki na hilo, watakachofanya ni kujituma na kufuta uteja wa klabu za nyumbani kushindwa kufanya vizuri zinapokutana na timu za waarabu.


"Sisi wachezaji tumejipanga vya kutosha kukabiliana nao na wao waje vizuri maana wakitudharau tutawaonesha maajabu kwani tuna dhamira ya kufika mbali mwaka huu." alisema Bocco

Azam wametinga hatua hiyo baada ya kuiondosha Bidvest Wits ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 7-3

Post a Comment

 
Top