BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda, Dar
TIMU za Yanga na Azam leo zimeshindwa kutambiana baada kutoka sare ya mabao 2-2 katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom uliopigwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam

Azam walikianza kipindi cha kwanza kwa shambulizi kali la dakika ya kwanza tu ambapo Kipre Tchetche aliingia eneo la hatari la Yanga lakini walinzi wa timu hiyo waliokoa na kutengeneza shambulizi kali langoni mwa Azam lakini halikuzaa matunda.Dakika ya 10 Tchetche alipiga shuti kali ambalo lilipanguliwa na kipa Ally Mustapha na mpira kumkuta mlinzi Juma Abdul ambaye alijifunga akiwa katika harakati za kuokoa.

Kosa kosa kwenye magoli ya timu zote ziliendelea hadi dakika ya 28 ambapo ilitokea piga nikupige langoni mwa Azam ndipo Juma aliporekebisha makosa yake kwa kuifungia Yanga bao la kusawazisha akifumua shuti kali nje ya eneo la 18.

Dakika ya 41, Mzimbabwe Donald Ngoma aliwainua vitini mashabiki wa Yanga kwa bao safi akimalizia kazi nzuri ya Amissi Tambwe.Kipindi cha pili Azam walionekana kulitafuta bao la kusawazisha kwa udi na uvumba ambapo kocha mwingereza Stewart Hall alimtoa Himid Mao na kumuingiza Frank Domayo ambaye alianzisha shambulizi kali lililozaa bao la kusawazisha. Bao hilo lililowafanya wababe hao wagawane pointi lilifungwa na John Bocco katika dakika 70.

Mabadiliko mengine kwa upande wa Azam ni Didier Kavumbagu aliyechukua nafasi ya Farid Mussa na Mudathir Yahaya aliyeingia badala ya Ramadhani Singano 'Messi'. Kwa upande wa Yanga, Hans Van Pluijm aliwatoa Simon Msuva na Tambwe huku nafasi zao zikichukuliwa na Geofrey Mwashiuya na Pato Ngonyani.

Kwa matokeo hayo Yanga inaendelea kuongoza ligi kwa kujikusanyia pointi 47 sawa na Azam ila inaizidi kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa. Kama Simba inayoshika nafasi ya tatu itashinda kesho dhidi ya Mbeya City, basi wekundu hao watakalia usukani wa ligi kwa mara nyingine.

Post a Comment

 
Top