BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Zainabu Rajabu, Chamazi


TIMU ya Azam leo imeutumia vema uwanja wake wa nyumbani wa Azam Complex baada ya kuichapa Stand United bao 1-0 katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom uliopigwa jioni ya leo jijini Dar es Salaam.

Stand ambao huu ni mchezo wao wa nne mfululizo wanapoteza, walionyesha uhai katika kipindi cha kwanza kwa kumudu kuwazuia Azam wasilete madhara langoni mwao huku nao wakifanya mashambulizi kadhaa langoni mwa Azam.

Hata hivyo Azam walifanikiwa kulifikia lango la Stand mara kadhaa na kama si kukosa umakini kwa washambuliaji wake Kipre Tchetche na Allan Wanga basi wangemaliza kipindi cha kwanza wakiwa wanaongoza.

Kipindi cha pili kocha Stewart Hall alifanya mabadiliko kwa kumtoa Wanga huku nafasi yake ikichukuliwa na John Bocco, mabadiliko ambayo yalizaa matunda kwani katika dakika ya 63, beki anayeongoza kwa mabao Tanzania, Shomari Kapombe aliipatia Azam bao la kwanza na pekee akimalizia krosi safi ya Bocco hili likiwa ni bao lake la nane msimu huu.

Baada ya bao hilo timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu lakini Azam walionekana kutawala zaidi mchezo huo na kulifikia lango la Stand mara nyingi zaidi.

Mabadiliko mengine kwa upande wa Azam ni Michael Balou aliyeingia badala ya Mudathir Yahaya huku Salum Waziri akichukua nafasi ya Farid Mussa. Kwa upande wa Stand, kocha Patrick Leiwig aliwapumzisha Amri Kiemba, Haruna Chanongo na Seleman Selembe, nafasi zao zikichukuliwa na Jeremia Juma, Vitalis Mayanga na Salum Kamana

Kwa ushindi huo Azam wamebakia nafasi ya tatu wakifikisha alama 50 sawa na Yanga ambao wanaizidi kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa. Simba wao wanaendelea kuongoza ligi wakijizolea alama 54 hadi sasa.

Post a Comment

 
Top