BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda

KIUNGO wa Taifa Stars na timu ya Simba, Mwinyi Kazimoto amewatoa hofu watanzania kwa kusema kuwa anaendelea vizuri baada ya kuumia nyonga katika dakika ya 46 ya mchezo kati ya Chad na Stars uliochezwa jioni ya leo jijini D'jamena.

Kazimoto aliyepangwa katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo iliyoibuka na ushindi wa bao 1-0, alipata maumivu makali yaliyompelelea kutolewa uwanjani kwenye dakika ya 46 ya mchezo huku nafasi yake ikichukuliwa na John Bocco.

Baada ya mchezo huo Kazimoto aliiambia BOIPLUS kuwa alipata maumivu makali lakini kadiri muda unavyokwenda anazidi kujisikia vizuri.

"Pale uwanjani nilipata maumivu makali sana ya nyonga hadi nikashindwa kuendelea na mchezo, lakini sasa naendelea vizuri na hata daktari ameniambia sio tatizo kubwa sana." alisema Kazimoto

Akizungumzia mchezo wa marudiano na Chad utakaopigwa kwenye dimba la Taifa mwishoni mwa juma hili Kazimoto alisema kwa anavyojisikia sasa anaona kuna uwezekano mkubwa wa yeye kucheza kama tu mwalimu atampa nafasi.

Stars itarejea nchini kesho usiku ikitokea Chad na kuingia kambini moja kwa moja kujiandaa na mchezo wa marudiano ambao kama watashinda basi watakuwa wamejizolea pointi saba.

Post a Comment

 
Top