BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda


TIMU za Barcelona ya Hispania na Bayern Munich ya Ujerumani zimeibuka na ushindi katika mechi zake za marudiano dhidi ya Arsenal na Juventus kwenye michuano ya klabu bingwa barani Ulaya.

Barcelona ambayo iliishindilia Arsenal mabao 2-0 kwenye mchezo wa kwanza, imeitupa nje ya michuano hiyo kwa jumla ya mabao 5-1 baada ya leo kuitandika mabao 3-1 kwenye uwanja wa Nou Camp.

Barca ilipata bao la kwanza katika dakika ya 18 kupitia kwa Neymar Jr akimalizia kazi nzuri ya Luis Suarez kabla Mohamed Elneny hajaisawazishia Arsenal kwenye dakika ya 51 akitumia pasi nzuri ya Alexis Sanchez.

Katika dakika ya 65, Suarez aliipatia Barca bao la pili kwa msaada wa beki wa kulia Daniel Alves kabla Lionel Messi hajashindilia msumari wa mwisho kwenye dakika 88.

Juventus ambayo ililazimishwa sare ya mabao 2-2 na Bayer kwenye mchezo wa awali, leo imekubali kichapo cha mabao 4-2 ugenini hivyo kuondolewa kwa jumla ya mabao 6-4

Paul Pogba aliwahi kutingisha nyavu za Bayern katika dakika ya tano tu akimalizia kazi nzuri ya Stephan Lichtstesteiner halaf Juan Quadrado akamalizia pasi ya Alvaro Morata ambaye alikimbia na mpira toka nje ya 18 na kuipatia Juve bao la pili.

Robert Lewandowski aliifungia Bayern bao la kwanza kwenye dakika ya 73 na wakati watu wanaanza kuinuka vitini, mkongwe Thomas Muller aliwapa furaha mashabiki wa Bayern baada ya kuisawazishia bao katika dakika ya 90 hali iliyopelekea mchezo huo uingie kwenye dakika 30 za nyongeza.

Katika dakika ya 108, Thiago Alcantara aliipatia Bayern bao la tatu ambapo dakika mbili baadaye Kingsley Coman aliongeza bao la nne kwa upande wa wajerumani hao.

Post a Comment

 
Top