BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Zainabu Rajabu, Dar

YANGA inajipa jeuri ya kuifunga Azam FC kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara baada ya kuwa wababe wa Simba msimu huu kwani wamewapiga nje ndani ila nahodha wa Azam, John Bocco amesema wataishusha Yanga kileleni kwenye mechi yao ya Jumamosi.

Timu hizo ambazo zote zimeingia hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la FA zitacheza mechi hiyo ya ligi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo mzunguko wa kwanza timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.

Bocco ametamba kuwa kikosi chao ni bora na imara ikiwa ni pamoja na benchi lao la ufundi hivyo kazi yao ni kuonyesha kwa vitendo na si maneno kama ilivyo upande wa pili kwa maana ya Yanga.

"Nguvu zangu na wenzangu tumezielekeza kwenye mechi hiyo ijayo ya Yanga, tumejipanga kuwanonyesha kazi kwani tumedhamiria kushinda mchezo huo ili kutwaa ubingwa wa ligi," alisema Bocco

Wakati Bocco akitamba kuisambaratisha Yanga, Kocha Msaidizi, Denis Kitambi amesema kuwa wachezaji wao wapo katika hali nzuri na ya ushindani hivyo wanaamini watashinda mechi hiyo.

Azam wao wametua leo jijini Dar es Salaam wakitokea Moshi ambako walikuwa na mechi ya Kombe la FA ambapo waliifunga Panone FC bao 2-1 na wameweka kambi yao kwenye hosteli ya timu hiyo iliyopo Chamazi wakati Yanga wao wamekimbilia Pemba.

Timu hizo zote zina pointi 46 lakini zina tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa ambapo Yanga ndiyo ipo kileleni wakati Azam inashika nafasi ya pili, msimamo huo wa ligi unaifanya ligi iwe ngumu na upinzani mkubwa kwani mpaka sasa bado haijajulikana nani atatwaa ubingwa huo.

Post a Comment

 
Top