BOIPLUS SPORTS BLOG

Manchester, Uingereza
KINDA wa Manchester United, Marcus Rashford ameendelea kung'ara katika kikosi cha mashetani hao baada ya jana kuiwezesha timu yake kuibuka na ushindi wa bao 1-0 kwenye uwanja wa Etihanld jijini Manchester.

Mechi hiyo ya wapinzani wa jadi wa jiji la Manchester inayofahamika kwa jina la 'Manchester Derby' iliamuliwa na bwana mdogo huyo katika dakika ya 16 tu ya mchezo alipopokea pasi ya Juan Matta na kumlamba chenga beki wa City kabla hajamchambua kipa Joe Hart na kuupachika mpira wavuni.

Liverpool wakiwa wageni wa Southampton walipata mabao mawili ya haraka haraka kupitia kwa Philipe Coutinho na Daniel Sturridge katika dakika za 17 na 22 hivyo kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao hayo mawili.

Kipindi cha pili wenyeji walipata penati ambayo ilipigwa na Sadio Mane ambaye alikosa. Southampton hawakukata tamaa, waliendelea kufanya mipango ambayo ilifana katika dakika ya 64 ambapo Mane alifuta makosa yake kwa kuifungia bao timu yake.

Dakika 20 baada ya bao hilo, Graziano Pelle aliisawazishia Southampton kabla Mane hajaithibitishia timu yake pointi tatu kwa bao safi la dakika 86 na kuwaondoa vichwa chini watoto wa Jurgen Klopp.

Kwa matokeo hayo City wameendelea kubaki katika nafasi ya nne wakifikisha pointi 51, United ipo nafasi ya sita kwa pointi 50 walizojikusanyia. Southampton wenyewe wapo kwenye nafasi ya saba wakiweka kibindoni pointi 47 na Liverpool wana pointi 44 wakimiliki eneo kwenye nafasi ya tisa.

Post a Comment

 
Top