BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda, Dar


MSHAMBULIAJI kinda wa Simba, Hija Ugando ambaye alitumia muda mfupi sana kumshawishi kocha Jackson Mayanja kumjumuisha kwenye kikosi cha kwanza cha wekundu hao, ameanza mazoezi rasmi juzi.

Hija ambaye aliumia nyonga katika mazoezi ya mwisho kabla ya kuivaa Yanga aliiambia BOIPLUS kuwa sasa anaendelea vizuri na amepangiwa program ya mazoezi ya ufukweni kwa muda wa wiki moja kabla hajajiunga wa wenzake.

"Niliumia nyonga wakati tunajiandaa na mechi dhidi ya Yanga ila sasa naendelea fresh, nimeanza mazoezi Coco Beach juzi, nitapiga wiki moja ndo niingie uwanjani." alisema Hija ambaye anapendelea kushambulia akitokea pembeni.

Akizungumzia nafasi yake kwenye kikosi cha kwanza mara atakaporejea, Hija alikiri kuwa ana kazi kubwa ya kufanya lakini akasema atarudi kwa nguvu kubwa.

"Najua ni kazi ngumu kwa mchezaji kurudi kwenye kiwango chako cha kawaida baada ya kutoka kwenye majeruhi, lakini nitapambana niwe fit haraka iwezekanavyo."

Simba inayoongoza ligi ikiwa imejikusanyia pointi 54, inajiandaa na mchezo wake wa ligi kuu dhidi ya Coastal Union utakaopigwa kwenye dimba la Mkwakwani jijini Tanga.

Post a Comment

 
Top